Habari

Wizara ya Uwekezaji Ondoeni Vikwazo, Tanzania Sio Kisiwa; Rais Samia

Katika hotuba yake Rais Samia amekiri kwamba wawekezaji wamekuwa wakillalamikia urasimu na mambo mengine ambayo yanafanya Tanzania kuonekana kama taifa lisilotabirika na kupunguza kasi ya uwekezaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameziagiza Wizara ya Ofisi Ya Waziri Mkuu, Uwekezaji pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha wawekezaji nchini Tanzania.

 

Ametoa maagizo hayo leo Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es salaam, baada ya kuwaapisha watendaji wa wizara ambao ni makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali.

 

Mhe. Rais amesema “tunataka wawekezaji wa-enjoy [wafurahie] Tanzania, makampuni yanafungwa ndugu zangu sio uongo, tukiweka vikwazo tunawarudisha nyuma, wakiondoka uchumi wetu unashuka, ajira zinapungua na mzunguko wa pesa unapungua, hiki ni kilio kikubwa cha watanzania kuwa mifuko mitupu.”

 

Aidha, amekitaka Kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania (TIC) kuhakikisha inaunganisha utendaji wa vitengo vyote vya serikali ambavyo mwekezaji anapaswa kujisajili ili kuondoa urasimu ambao umekuwa kikwazo kikubwa kwa wawekezaji.

 

Katika hotuba yake Rais Samia amekiri kwamba wawekezaji wamekuwa wakillalamikia urasimu na mambo mengine ambayo yanafanya Tanzania kuonekana kama taifa lisilotabirika na kupunguza kasi ya uwekezaji.

 

Je, unadhani kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan itaibua tumaini jipya kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Tanzania?