Habari

Waziri Ndugulile: Tozo za Usajili wa Blogs, Online TV Zipunguzwe

Waziri amewataka TCRA kupunguza gharama za usajili wa mitandao ya kijamii ili vijana waweze kujiajiri kupitia mitandao hiyo ambapo alitoa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha Sheria zote zimepitiwa na muda wa usajili wa mitandao hiyo umefunguliwa

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mkoani Arusha alipokutembelea taasisi za wizara hiyo na kusema  kuwa ni vyema mamlaka hiyo ikajikita zaidi kutoa Elimu kwa jamii kwani ni kosa kisheria kuendesha vyombo vya habari vya kimtandao (blogu na TV) bila kusajiliwa.

Waziri amewataka TCRA kupunguza gharama za usajili wa blogu na TV za mtandaoni ili vijana waweze kujiajiri kupitia mitandao hiyo ambapo alitoa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha sheria zote zimepitiwa na usajili kuendelea tena baada ya kusitishwa.

Katika hatua nyingine Waziri alitumia nafasi hiyo kuwaasa mafundi simu wote wenye tabia za kufuata namba ya kipekee inayotambulisha simu husika (IMEI) wanapopelekewa simu kwa ajili ya matengenezo na kuwaasa kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.


“Baadhi ya mafundi simu wasio waaminifu wanatumika kufuta IMEI (International Mobile Equipment Identity) namba za simu za mkononi za wateja wao ili simu hizo ziweze kutumika tena kitendo ambacho ni kosa kisheria na serikali itawachukulia hatua kali mafundi watakaobainika kufanya tabia hiyo” alisema Ndugulile.

Kwa upande wake meneja wa mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Kaskazini,  Mhandisi Emelda Salumu alisema kuwa mamlaka ya mawasiliano Tanzania kwa upande wa Kanda hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wana mpango wa kukusanya kiasi cha shilingi billioni 1.27 ambapo hadi sasa wamekusanya kiasi cha zaidi ya shilingi millioni 800.

Alisema katika kuhakikisha uhalifu kupitia mitandao ya simu unapungua wameamua kutoa elimu kwa wananchi pamoja na mafundi simu ambapo jumla ya mafundi 332 wamepatiwa mafunzo kwa upande wa Kanda ya kaskazini ambapo kwa upande wa Kilimanjaro jumla ya mafundi 67 wamepatiwa mafunzo, Arusha 133, Tanga 67 na Manyara 78 ambapo kwa Manyara bado wapi kwenye mafunzo.

“Mafunzo haya yatawasaidia kuwa wafanisi Katika kazi zao pia wataona utofauti yao waliopewa mafunzo pamoja na wale ambao hawakupewa mafunzo.” Alisema.