Habari

Watatu Mbaroni kwa Usafirishaji wa Vinyonga na Nyoka Kinyemela

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alisema vinyonga na nyoka hao walikamatwa na maofisa wa forodha wa Austria wakiwa wamewekwa kwenye begi huku wakiwa wamefunikwa kwa soksi na vifungashio vya plastiki

Watanzania watatu watiwa mbaroni kwa wakituhumiwa kushirikiana na Jamhuri ya Czech wakituhumiwa kusafirisha nje ya nchi vinyonga 74 na nyoka 6.

Kupitia vyombo vya habari jana Machi 11, 2021 mkoani Iringa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alisema vinyonga na nyoka hao walikamatwa na maofisa wa forodha wa Austria wakiwa wamewekwa kwenye begi huku wakiwa wamefunikwa kwa soksi na vifungashio vya plastiki.

Alisema vinyonga na nyoka hao waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Vienna nchini Austria, inadaiwa wametoka Tanzania katika Milima ya Usambara ambako kuna aina mbalimbali za vinyonga.

 Dk Ndumbaro amesema baada ya kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, wizara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na kwa kutumia kikosi kazi Taifa dhidi ujangili iliunda kikosi maalum cha kuchunguza tukio hilo na  kupitia taarifa za kiintelijensia, kikosi maalum kilifanikiwa kupata jina la mtuhumiwa aliyesafirisha vinyonga hao ambaye ni raia wa Jamhuri ya Czech.

Aidha, Dk. Ndumbaru ameweka wazi kuwa watuhumiwa wanatarajia kufikishwa mahakamani

Kesho na kwamba, watakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha nje wanyapori bila kibali, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha huku akiahidi kuwasiliana na serikali ya jamhuri ya Czech ili raia wa kule waliohusika nao wachukuliwe hatua.

Wakati huohuo, Dk Ndumbaro amesema Serikali inakusudia kuifuta biashara ya wanyamapori hai ambayo ilizuiwa tangu Mei 2016.

Amesisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya biashara ya wanyamapori hai ndani na nje ya nchi na mtu yoyote atakayebainika kufanya biashara hiyo wakati imezuiliwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kukamatwa kwa raia hao ni utekelezaji wa tamko walilolitoa hivi karibuni baada ya kubaini ushikiliwaji kinyemela wa vinyonga hao nchini Austria.

Hivi karibuni, Wizara ya Maliasili na Utalii ilisema kuwa inafanya jitihada kuwarejesha vinyonga waliokamatwa nchini Austria ambao walisafirishwa kinyemela mwezi January huku zikibainisha kuwa tayari watanzania wawili walikuwa mbaroni kwa ajili ya uchunguzi.