Burudani

Wasanii wa Kike Tanzania Wanaotamba YouTube, Zuchu Kileleni Ndani ya Mwaka Mmoja

Nandy, na Vanessa Mdee na Maua Sama wanafuata kwa Mbali

Biashara ya maudhui ya muziki mtandaoni kwa njia ya kusikilizwa na kutazamwa imeendelea kukua, huku wasanii kote duniani wakiendelea kuwekeza kwenye namna mbalimbali za kuongeza usikilizwaji katika mitandao kama YouTube, Deezer, Apple Music, Audiomack, YouTube Music, Boomplay Music, Pandora, Spotify, Tidal na kadhalika.

 

Katika kufanya hivyo, wasanii wengi duniani wamekuwa mamilionea kama si mabilionea kutokana na mapato ya uuzaji muziki kwa njia hizo.

 

Tanzania imekuwa kwenye orodha ya nchi barani Afrika ambazo wasanii wake wamekuwa wakiongoza kwenye kusikilizwa na kutazamwa kwenye mtandao wa YouTube miongoni mwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Katika machapisho ya hivi karibuni, wasanii kutoka Tanzania kama Diamond Platnumz, Harmonize, Rayvanny, Mbosso na Lavalava wametajwa na Billboard kama miongoni mwa wale wanaofanya vizuri zaidi kwenye kusikilizwa na kutazamwa kupitia jukwaa la YouTube.

 

Pengine hatukuwahi kujiuliza, lakini katika orodha hizi ni kwanini wasanii wa kike hawaonekani? Tumefikiria tuanzie ndani kwa kutupia jicho kwenye utendaji kazi wa wasanii wa kike mtandaoni. Leo tumekuandalia orodha ya wasanii wa kike Tanzania ambao idhaa zao za mtandao wa YouTube zinaongoza kwa kutazamwa zaidi, kwa kuangalia jumla ya mara zote ambazo idhaa hizo zimetembelewa.

 

Katika kuangazia orodha hiyo, jambo linaloweza kushangaza ni kuwa, msanii kutoka lebo ya WCB, Zuhura Othman Soud, maarufu kama Zuchu ambaye bado hajatimiza mwaka mmoja tangu ameingia kwenye kiwanda cha muziki anaongoza orodha hiyo na kuwaacha maili nyingi wasanii wenzake wa kike wakongwe.

 

1. Zuchu- 103,202,342 

Zuchu ni msanii mpya kwenye kiwanda cha muziki Tanzania akitokea lebo ya Muziki ya WCB chini ya Diamond Platnumz. Zuchu alitambulishwa mwanzoni mwa mwaka wa 2020, na hadi kufikia sasa ametazamwa mara 103,202,342 (milioni 103.2) ambayo inamfanya awe msanii wa kike Tanzania anayeongoza kwa idhaa yake kutembelewa zaidi katika historia ya muziki wa BongoFleva.

 

Idhaa ya YouTube ya mkali wa 'Sukari' ilifunguliwa Januari 29, 2019.

 

2. Nandy- 91,568,549

Nandy ni Nandy. Ni msanii mkubwa Tanzania na Afrika Mashariki na ameshajizolea tuzo kadhaa na kufanya matamasha ndani na nje ya nchi. Hadi tunakwenda mitamboni, idhaa ya YouTube ya Nandy imetazamwa mara 91,568,549 (milioni 91.5) na kumfanya kuwa msanii wa pili aliyetazamwa au kusikilizwa zaidi Tanzania.

 

Idhaa ya YouTube ya Nandy anayetamba kwa 'Number One' ilianzishwa Julai 5, 2016

 

3. Vanessa Mdee- 38,672,430

Vanessa Mdee ni jina kubwa si tu Tanzania, bali hata duniani anafahamika. Nje ya muziki, Vanessa amevuma mitandao kupitia mahusiano yake baada ya kuvishwa pete ya uchumba na Rotimi, Mmarekani mwenye asili ya Nigeria. Vanessa Mdee amekuwa ni mwimbaji mwenye mafanikio ya kuridhisha tangu alipoingia rasmi kwenye sanaa ya muziki na amejizolea umaarufu Tanzania na barani Afrika.

 

Hadi kufikia sasa, idhaa ya Vanessa Mdee ya YouTube imejizolea utazamaji na usikilizaji 38,672,430 na kumfanya awe msanii wa tatu katika orodha hii.

 

Idhaa ya YouTube ya Vanessa Mdee ambaye mwaka 2020 alitangaza kuupa kisogo muziki ilianzishwa Oktoba 11, 2011

 

4. Maua Sama- 31,574,705

Maua anaimba, na anaimba vizuri. Msanii huyo aliyetambulishwa kiwandani na MwanaFA anasifika kwa uwezo wake wa uimbaji na utunzi wa mashairi akiwa ametoa nyimbo nyingi zilizopata mafanikio ya kuridhisha katika muziki wa Tanzania.

 

Hadi kufikia sasa, idhaa ya Maua Sama imetazamwa mara 31,574,705 na kumfanya ashikilie namba nne katika orodha hii ya wasanii wa kike Tanzania.

 

Idhaa ya YouTube ya Maua Sama, mkali wa 'Iokote' ilianzishwa Januari16, 2015

 

5. Queen Darleen- 15,751,510

Queen Darleen, ni msanii aliyesajiliwa na Lebo ya WCB chini ya Diamond Platnumz. Kabla ya sakata la ‘Mama Dangote’ kumuibua ‘baba mzazi mpya’ wa Diamond Platnumz, wengi walimfahamu Queen Darleen kama mtoto wa Baba mmoja na Diamond Platnumz.

 

Tangu kusajiliwa na WCB na kuanza kuitumia idhaa yake, Queen Darleen amejikusanyia jumla ya utazamaji 15,751,510 katika idhaa yake.

 

Idhaa ya Queen Darleen 'First Lady wa Wasafi' ilifunguliwa Novemba 9, 2017

 

6. Ruby- 11,710,093

Ruby ni msanii anayefahamika kwa uwezo wake wa hali ya juu wa uimbaji, mtaani husema kuwa anaweza kumtoa nyoka pangoni pale afunguapo kinywa kuimba.

 

Ruby amekuwa na misukosuko mingi, huku nyimbo zake nyingi zikiwa zimepandishwa katika idhaa nyinginezo kama Africori, BMM Music Group na THT jambo ambalo limeminya nafasi yake ya kuwa juu kwenye orodha hii.

 

Katika idhaa ambayo hata hivyo inaonekana imeacha kutumika, Ruby ana utazamaji wa 11,710,093. Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, msanii Ruby anaonekana kufungua idhaa nyingine ya YouTube ambayo imeweka wimbo wake mpya aliotoa wiki chache zilizopita.

 

Idhaa hii ya YouTube ya Ruby, 'mkali wa masauti' ilifunguliwa Oktoba 26, 2016.

 

7. Lady Jaydee - 10,870,064 

Lady Jaydee, wengi wanamuita Malikia wa BongoFleva kutokana na histori ndefu ndani ya kiwanda. Lady Jay Dee ni miongoni mwa wasanii wa kike ambao wameutoa muziki mbali, na wameendelea kuwepo takribani miongo miwili baadaye huku Maisha yake yakiwa hayajaambatana na kashfa kama ilivyo kwa wasanii wengine wengi.

 

Jay Dee ana jumla ya utazamaji 10,870,064, idadi inayomfanya ashike namba 7 katika orodha hii. Hata hivyo, mtapanyiko wa nyimbo za Lady Jaydee ni moja ya sababu inayofanya kutapanyika kwa watazamaji wake. 

 

Idhaa ya YouTube ya 'Komando' Jay Dee ilifunguliwa Aprili 6, 2016.

 

8. Shilole - 9,690,428 

Shilole tunaye! Shilole alianza kama muigizaji wa filamu na baadaye kuhamia kwenye muziki alipopata mafanikio. Hivi sasa, Shilole ni mfanyabiashara mkubwa wa huduma ya mghahawa ambayo amenukuliwa akisema imempa mafanikio ikiwamo kununua gari la kifahari na kujenga nyumba ya kisasa.

 

Idhaa ya YouTube ya Shilole ina jumla ya watazamaji 9,690,428 hadi kufikia tarehe ya kuandikwa makala haya.

 

Idhaa ya YouTube ya Shilole ilifunguliwa Januari 31, 2016.

 

8. Rosa Ree - 8,177,989

Rosa Ree ni msanii wa Hip Hop wa kike anayefanya vizuri Tanzania, pengine ndiye anayeongoza kwa sasa.

Kabla ya kuwa ‘solo’, Rosa Ree alikuwa chini ya The Industry, lebo inayosimamiwa na Navy Kenzo (Nahreel na Aika)

 

Hadi kufikia sasa, Rosa Ree kupitia idhaa yake ya YouTube amejikusanyia utazamaji 8,177,989 na kumfanya awe msanii wa nane katika orodha hii.

 

Idhaa ya YouTube ya Rosa Ree ilifunguliwa Machi 5, 2015

 

9. Amber Lulu- 7,963,544

Hakuna mengi sana ya kusema kuhusu Amber Lulu ila alipoanza kuimba watu wengi walimchukulia kiutani tu na hawakumpa usikivu alioutaka. Amber Lulu amefanikiwa kutoa nyimbo kadhaa zilizopata usikilizaji mzuri kutoka kwa mashabiki wa Bongo Fleva.

 

Hadi kufikia sasa, idhaa ya Amber Lulu imetazamwa mara 7,963,544 na kumfanya ashike namba tisa katika orodha hii ya wasanii wa Bongofleva.

 

Idhaa ya YouTube ya Amber Lulu ilifunguliwa Disemba 27, 2016.

 

10. Linah Sanga- 7,845,875

Linah Sanga tunaye kwa muda mrefu sasa. Ni msanii aliyelelewa na THT chini ya aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media Group, marehemu Ruge Mutahaba.

 

Linah amekuwa kwenye mwanga kwa muda mrefu sasa, na amepata mafanikio yanayomfanya afahamike katika kiwanda cha muziki cha Tanzania.

 

Hadi kufikia sasa, Linah Sanga amejikusanyia utazamaji milioni 7,845,875 kwenye idhaa yake ya YouTube. Mkali wa 'Kilegeze' ni moja ya wasanii wanaokabiliwa na ombwe la usimamizi imara mtandaoni kwani namba aliyopo haiendani na ukubwa wa kazi yake. 

 

Idhaa ya YouTube ya Linah Sanga ilifunguliwa Julai 10, 2014.

 

Je, orodha hii imefanikiwa kuwapata wote au kuna tuliowaacha? Usisite kuchangia kwenye eneo la maoni hapo chini, na kushiriki katika mitandao yetu ya kijamii.