Habari

Waandamanaji Wanaopinga Mapinduzi ya Kijeshi Myanmar Wakumbwa na Maji ya Kuwasha

Wito wa kujiunga na maandamano umekua zaidi na kupangwa zaidi tangu mapinduzi yalipotokea Jumatatu iliyopita huku wanajeshi wakifunga mitandao ya kijamii ili isitumiwe na wapinzani

Februari 8, watu kutoka pande zote za  Myanmar walijiunga katika siku ya tatu ya maandamano ambayo yalianza kupata nguvu katika mji mkuu wa Yangon siku ya Jumamosi, yakienea hadi kwenye miji mingine jana Jumapili huku wakilenga kupinga mapinduzi ya kijeshi na kutoa wito wa kuachiwa kwa kiongozi wa taifa hilo Aung San Suu Kyi.

Wakati maandamano yakiendelea Jeshi la nchi hiyo lilisambaza idadi kubwa ya askari wa kutuliza ghasia katika mji mkuu, Naypyidaw huku wakiwarushia maji yaliyochanganywa kemikali dhidi ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi.

Jeshi la nchi hiyo linakabiliwa na shinikizo kutoka kwenye mataifa mbalimbali huku wakiendelea kushikilia msimamo wao kuwa walihalalisha mapinduzi kutokana na  madai ya udanganyifu katika uchaguzi uliopita wa Novemba, ambao chama cha Suu Kyi (NLD) kilishinda kwa kishindo.

Jumuiya hiyo imetangaza hali ya dharura inayodumu kwa mwaka na kuahidi kufanya uchaguzi mpya - bila kutolewa kwa muda maalum.

Wakati mapinduzi hayo yakilaaniwa kimataifa, China, mshirika wa kikanda na kiuchumi imekataa kukosoa majenerali waliosimamia mapinduzi hayo.

Wito wa kujiunga na maandamano umekua zaidi na kupangwa zaidi tangu mapinduzi yalipotokea jumatatu iliyopita huku wanajeshi wakifunga mitandao ya kijamii ili isitumiwe na wapinzani.

Pamoja na mamlaka ya kijeshi kuzima mara kwa mara waandamanaji wa mtandao walilazimika kurejea kwa simu na ujumbe wa maandishi kuandaa maandamano.

Myanmar, koloni la zamani la waingereza wakati huo likijulikana kama Burma, lilikuwa chini ya utawala wa jeshi kwa miongo mitano kufuatia mapinduzi ya 1962.