Habari

Vatican: Mapenzi ya jinsia moja ni Chaguo Binafsi na sio Mapenzi ya Mungu

Vatican imetoa taarifa hiyo siku ya jumatatu ikitilia mkazo kwamba Kanisa Katoliki halitabariki vyama vya watu wa jinsia moja, katika tamko lililoidhinishwa na Baba Mtakatifu, Francisko ambayo inatishia utengano kati ya kanisa hilo na sehemu kubwa ya jamii ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ).

Ikifafanua uamuzi wao kwa maandishi marefu Jumatatu, Vatikan ilitaja ushoga kama "chaguo binafsi", ikiuelezea muungano huo kama dhambi na ikasema "haiwezi kutambuliwa kama kitendo kilichoidhinishwa waziwazi" kwa mipango ya Mungu.

Papa Francis, ambaye amekuwa akisifiwa mara kwa mara kwa ukarimu wake kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ndani na nje ya Kanisa, aliidhinisha hati hiyo.

Uamuzi huo umewafadhaisha wakatoliki ambao walikuwa na matumaini kuwa taasisi hiyo ingeweza kuboresha namna ya kushughulika na mashoga." Sio sahihi kutoa baraka kwa uhusiano wa mapenzi kabla ya ndoa, hivyo haiwezi kuwa halali kwa wapenzi wa jinsia moja," ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema kwamba jamii hiyo kama walivyo binadamu wengine wanaweza kupata baraka ikiwa wataishi kulingana na mafundisho ya Kanisa.

Lakini kubariki vyama vya jinsia moja itakuwa ni sawa na kutuma ishara kwamba Kanisa Katoliki linaidhinisha na kuhimiza "chaguo na njia ya maisha ambayo haiwezi kutambuliwa kama ilivyoamriwa wazi kwa mipango iliyofunuliwa ya Mungu."

Taarifa hiyo ilitolewa kama "jibu" kwa maswali kutoka kwa wachungaji na waamini juu ya msimamo wa kanisa kuhusiana na jamii ya watu hao. Katika ufafanuzi uliotolewa na taarifa ya Jumatatu, Vatican ilisisitiza kwamba "mtazamo hasi juu ya kubariki vyama vya wapenzi wa jisia moja haimaanishi mtazamo hasi juu ya watu hao."

Wakati wa mahojiano mwaka jana, Papa alionekana kama alikuwa ametetea vyama vya kiraia vya wapenzi wa jinsia moja wakati alipotoa mahojiano ya maandishi.

Mashoga wana haki ya kuwa sehemu ya familia. Wao ni watoto wa Mungu na wana haki ya familia. Hakuna mtu anayepaswa kutengwa, au kujihisi mnyonge kwa sababu hiyo,” Papa Francis alisema.

Lakini Vatican upesi ilisahihisha kauli hiyo, ikisema imetafsiriwa nje ya muktadha na haikulenga kubadilidha kifungu chochote cha maandiko takatifu.