Tanzania

Ukatili wa Kingono Majumbani Nani Alaumiwe?

Tanzania waathirika wengi wanaofanyiwa ukatili wa kingono hawaongei wala kuwa wazi juu ya kile wanachofanyiwa na ukimya huu huwafanya waathirika wanaofanyiwa vitendo hivyo wakiwa bado watoto kuathirika kisaikolojia huku wakitafunwa na kumbukumbu mbaya za vitendo hivyo

Suala la ukatili wa kingono majumbani linazidi kuitafuna jamii ya leo, watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili huo wa kingono na watu wa karibu wanaomzunguka na wengine kutoka katika familia inaweza akawa baba, mjomba, kaka babu hata ndugu yeyote ndani ya familia au majirani.

Moja ya ukatili unaowakumba watoto ni pamoja na kubakwa kwa kudanganywa na zawadi ndogondogo huku wengine wakitishiwa kuuawa.

Tanzania waathirika wengi wanaofanyiwa ukatili wa kingono hawaongei wala kuwa wazi juu ya kile wanachofanyiwa na ukimya huu huwafanya waathirika wanaofanyiwa vitendo hivyo wakiwa bado watoto kuathirika kisaikolojia huku wakitafunwa na kumbukumbu mbaya za vitendo hivyo.

Kuna mambo mbalimbali ambayo yanachangia waathirika wa matukio ya ukatili kutoongea ukweli juu ya unyama huo wanaofanyiwa na mojawapo ikiwa ni kuogopa kudharirika, kuogopa adhabu wanazoambiwa na wale wanaowafanyia ukatili huku wengine maadili ya kidini ndani ya familia yanatengeneza mazingira ya hofu ya kuongea ukweli.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tanzania, Anna Henga katika mahojiano  juu ya  masahibu haya alieleza kuwa  suala la ukatili majumbani limekuwa  ni changamoto na  katika takwimu zao za miaka mitatu mfululizo zinaonesha kuwa ukatili wa kingono umekuwa ni mkubwa sana hasa kwa watoto na hufanywa na watu wao wa karibu ikiwemo wale wenye dhamana ya kuwatunza hata kuwalea.

Anna Henga anaihamasisha jamii yote kwa ujumla kuwa mstari wa mbele kuwalinda watoto hasa ambao wanaokutana na ukatili huu wa kingono majumbani.

Binti mmoja jijini Dar es salaam (jina linahidhifiwa) amewahi kukutana na ukatili wa kingono akiwa bado mtoto alipata wasaa wa kutuulezea masahibu hayo yasiyoweza kufutika kichwani mwake “ nataka nitoe stori ya  ukatili wa kijinsia  ambao nilifanyiwa nikiwa mdogo kwenye familia yangu na mtu ambaye alikuwa wa karibu sana, katika nyumba yetu kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu kuna vijana walikuwa wanakuja kushinda Binti nilikuwa peke angu na muda mwingi nilikuwa nabaki nyumbani  na dada wa kazi ambaye muda mwingi alikuwa yupo bize. Baba yangu mdogo alikuwa ananibaka ni kitendo ambacho nilikuwa sifurahii lakini nilikuwa sina sehemu ya kusema kwa sababu nilikuwa mdogo lakini pia wazazi wangu walikuwa ni watu wa dini sana  na kuongelea jambo hilo ingehitaji ujasiri wa kutosha hivyo hali iliendelea hivyo na hicho kitendo kiliendelea kwa muda na sio yeye tu, bali pia niliwahi fanyiwa kitendo hicho na kijana mmoja aliyekuwa jirani yetu alikuwa anafanya hivyo na kunidanganya kwa pipi.”

Kwa sasa nimegundua kuwa nilikuwa nafanyiwa unyama na kama ningesema kipindi kile huenda ningesaidia nakumbuka kila kitu hakifutika kichwani kwangu na ndiyo maana nikajiunga na harakati ili namimi niwasaidie wngine” alieleza.

Ikiwa huyo ni mmoja tu kati ya wanaofanyiwa ukatili amefunguka akiwa mkubwa je!  Niwangapi wanafanyiwa vitendo hivyo na hawasemi?

Binti mmoja aliwahi kufanyiwa ukatili wa kingono na babu yake huko Tanga na kupelekea kupata ujauzito akiwa darasa la sita hivyo alilazimika kuacha shule.

Kesi ya babu huyo ilifutiliwa mbali kutokana nguvu ya familia ili kulinda jina la ukoo.

Ukipita katika kurasa mbalimbali za kijamii hasa Facebook utakutana katika makundi mbalimbali ya ushauri utakutana na watu wakiomba ushauri juu   ukatili wanaokumbana nao majumbani na wengi ni wanawake wakiomba ushauri juu ya ukatili wanaofanyiwa watoto  wao na ndugu zao  majumbani huku wakisisitiza wafichwe majina yao.

Watu hawa hawapo tayari kuripoti matukio haya moja kwa moja katika sehemu za msaada wa kisheria hivyo kutumia muda mwingi mitandaoni kuomba ushauri.

Je! Kimya hiki juu ya Ukatili wa Kingono nani alaumiwe?


Imeandaliwa na 

Rachel Nzengo.