Habari

Twitter Yatupilia Mbali Agizo la Serikali ya India Likiwataka Wazifungie Akaunti 1,100 Zinazochochea Maandamano ya Wakulima

Licha ya kuwa hapo awali Mtandao huo wa kijamii uliondoa baadhi ya akaunti mapema wiki iliyopita, Twitter imesema inaamini agizo hilo linakiuka Sheria za India za Watu kuwa na uhuru wa kutoa maoni hivyo hawatozifungia

Kampuni ya Twitter imepuuza agizo la Waziri Mkuu wa India Narendra Modi la kuzifungia akaunti za Twitter ambazo anadai zinachochea maandamano ya Wakulima wanaolalamikia Sheria kuwakandamiza na kuwapa faida Wafanyabiashara.

Serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi ilitaka twitter iondoe akaunti zipatazo 1,100 na machapisho yanayosambaa mtandaoni yanayodai uongozi unawanyonya wakulima na kuongeza kuwa baadhi ya akaunti zinafadhiliwa na maadui zake kutoka Pakistan.

Licha ya kuwa hapo awali Mtandao huo wa kijamii uliondoa baadhi ya akaunti mapema wiki iliyopita, Twitter imesema inaamini agizo hilo linakiuka Sheria za India za Watu kuwa na uhuru wa kutoa maoni hivyo hawatozifungia.

Akielezea uamuzi wake katika chapisho la blogi, Mtandao wa twitter umeweka wazi kuwa uamuzi wake ni kwa lengo la "ni kutunza misingi na kutetea uhuru wa kujieleza".

Twitter imeripotiwa kuzifungia account zinazozidi 500 lakini ikaziacha zile za Wanaharakati, Waandishi na za Wanasiasa.

Wakulima nchini India wamekuwa wakiandamana nje ya mji mkuu, New Delhi, kutaka mageuzi ya kilimo tangu Novemba 26, licha ya kukumbana na vizuizi vya polisi.

Polisi wamesema maafisa 300 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo huku mamia ya waandamanaji wakiripotiwa kujeruhiwa na kifo cha mkulima mwenye umri wa miaka 26 ambaye trekta lake lilipinduka baada ya kugonga kizuizi cha polisi.

Serikali imeamua kuzima mtandao katika maeneo ya nchi hiyo ikiwa ni juhudi za kuzuia maandamano, hatua inayotumiwa mara kwa mara kuzuia wapinzani.