Habari

Trump Akana Uvumi wa Kuanzisha Chama Kipya

Bw.Trump amesema hayo akiwa katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina CPAC uliofanyika mjini Orlando katika jimbo la Florida akidai kuwa kitendo cha kuanzisha Chama kipya kitagawanya kura za Republican na kupelekea chama hicho kisishinde tena

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump amezungumza kwa mara ya kwanza tangu Joe Biden akabidhiwe madaraka kama Rais na kusema hana mpango wa kuanzisha Chama kipya cha Siasa

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina CPAC uliofanyika mjini Orlando katika jimbo la Florida, mwanachama huyo wa Republican amesema kitendo cha kuanzisha Chama kipya kitagawanya kura za Republican na kupelekea chama hicho kisishinde tena.

Trump alianza hotuba yake kwa kuwaambia wasikilizaji kwamba, licha ya uvumi, hakuwa na mpango wa kuanzisha chama kipya. Alisema hamna ulazima kwani kwani yeye ni tayari mwanachama wa Republican.

Ingawa muda mwingi katika mkutano huo alitumia kukosoa sera za utawala wa Rais Biden na chama cha Democratic kuwa umefeli kwenye maeneo mengi ikiwa ni wiki chache tu baada ya kuingia madarakani. Aidha, Katika mkutano huo Bw. Trump amedokeza kuwa huenda akagombea tena kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2024.

Akiashiria uwezekano huo, Trump aliyeiongoza Marekani kwa muhula mmoja kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 amesema:

"Nani anayejua. Ninaweza kuamua kuwashinda kwa mara ya tatu. Hio ni sawa?

Trump pia aliendelea kusisisitiza madai yake yasiokuwa na ushahidi kuwa alimshinda rais wa sasa Joe Biden katika uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka uliopita.

Hotuba hiyo inakuja wiki kadhaa baada ya Bw Trump kuachiliwa huru kutoka kesi ya mashtaka dhidi yake iliyokuwa inamkabili.

Kuonekana kwake katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina (CPAC) huko Orlando Jumapili ilikuwa ishara ya ushawishi wake unaoendelea juu ya Chama cha Republican.Mkutano huo wa kila mwaka hufanyika mjini Washington lakini ulihamishwa hadi Orlando kutokana na vizuizi vya Covid-19 vilivyowekwa mjini Florida.