Habari

Sudan Yatangaza Hali ya Hatari Magharibi mwa Darfur

Mashuhuda walisema milio ya risasi ilisikika katika vitongoji vya Hay Al Jabal na Al Jamarik jioni ya Jumatatu

Sudan imetangaza hali ya hatari katika jimbo la Darfur Magharibi kufuatia mapigano ya kikabila ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 40 na maelfu ya watu wakiachwa bila makazi na wengine wakikimbia majumbani mwao.

 

Siku ya Jumatatu, UN ilisema kwamba watu wasiopungua 40 waliuawa na zaidi ya 50 walijeruhiwa baada ya ghasia kuzuka Jumamosi kati ya vikundi vya Kiarabu na jamii isiyo ya Kiarabu ya Massalit katika jiji la El Geneina.

Mashuhuda walisema “milio ya risasi ilisikika katika vitongoji vya Hay Al Jabal na Al Jamarik jioni ya Jumatatu.”

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu linasema shughuli za kibinadamu zimesimamishwa na safari za ndege za kibinadamu zimefutwa hadi hali ya usalama itakapoboresha. Hali imebaki kuwa ya wasiwasi na hatari katika mji huo huku pande zote mbili zikiwa zinakusanya vikosi vyao kuongeza nguvu.

 

Aidha, jiji hilo lilikuwa kitovu cha kupeleka misaada na zaidi ya watu 700,000 ambao wameathiriwa na kuzorota kwa hali ya usalama, hayo yamesemwa na ripoti ya Umoja wa Mataifa.

 

Mnamo Januari, kati ya Massalit na jamii za Kiarabu ulisababisha vifo vya watu wasiopungua 129 na kuhama makazi yao zaidi ya watu 108,000 - na wengi wao wakiwa wamehifadhiwa mashuleni na katika vituo vya afya katika mji huo.