
Mkutano wa usalama wa Munich ulifanyika kwa njia ya video hapo jana, Februari
19 ukihusisha washirika kutoka mataifa 7 tajiri zaidi duniani.
Rais Joe Biden katika hotuba yake kwenye
mkutano wa Munich wa masuala ya usalama uliofanyika kwa njia ya video, ameahidi
kwamba Marekani itashirikiana na washirika wake wa Ulaya katika juhudi za
kukabiliana na changamoto zilizopo, ikiwa pamoja na janga la maambukizi ya
corona, ugaidi na mabadiliko ya tabia nchi. Mkutano huo wa Munich wa masuala ya
usalama hufanyika kwenye mji huo wa Ujerumani kila mwaka
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa
Ufaransa Emmanuel Macron na mwenyekiti wa zamu, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris
Johnson. Washiriki wengine walikuwa, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya,
Ursula von der Leyen, katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Yaliyojiri katika mkutano huo:
1. 1. Biden
ametangaza Mwisho wa mtindo diplomasia wa Trump 'Marekani Kwanza'
"Marekani imerudi, muungano kati yake na
nchi za bara la Ulaya umerudi," Bwana Biden alitangaza. Akijaribu
kufutilia mbali miaka minne iliyopita bila hata kumtaja mtangulizi wake, Donald
J. Trump, Bwana Biden alisema "hatutazami nyuma."
Pia ameonesha nia yake ya kutaka kutetea na
kuilinda demokrasia ya nchi yake na kudai kuwa hiyo ndiyo dhamira yake kubwa na
kwamba demokrasia haitokei kwa bahati mbaya lazima itetewe, iimarishwe, ilindwe
na iendane na mabadiliko ya sasa.
Lakini pia ameishinikiza Ulaya kufikiria namna
ya kutatua changamoto kwa njia mpya - ambayo inatofautiana na ile ya Vita
Baridi ingawa wapinzani wao wawili (china na Urusi) wanajulikana toka kipindi
hicho.
"Lazima tujiandae pamoja kwa ushindani wa
kimkakati wa muda mrefu na nchi ya China," alisema, akitaja "Cyberspace,
ujasusi bandia na bioteknolojia" kama mambo muhimu katika ushindani. Nchi
za magharibi lazima ziweke sheria za jinsi teknolojia hizi zinatumiwa, alisema,
badala ya kuiachia Beijing pekee katika kufanya maamuzi.
2. Viongozi wa Ulimwengu Wapanga Mkakati Mpya Baada Utawala wa Bw.Trump
Akiongea katika video Waziri Mkuu wa
Uingereza, Boris Johnson aliitisha wito kwa viongozi wa Kundi la mataifa 7
Ijumaa alasiri, kushinikiza ushirikiano zaidi na uratibu wa kusambaza chanjo za
virusi vya corona kwa mabilioni ya watu katika nchi zinazoendelea.
Katika wito huo, Waziri Johnson aliahidi
kwamba Uingereza itatoa misaada ya ziada ya chanjo kwa mpango ambao utasambaza
dozi katika nchi zinazoendelea. Bwana Biden pia alithibitisha kuwa Marekani
itatoa dola bilioni 4 kuunga mkono juhudi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
3. Merkel ataka mkakati wa pamoja katika kushughulikia China na Urusi
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alitoa
wito kwa Marekani na Ulaya kutafuta njia ya pamoja ya kushughulika na China na
Urusi, akiongeza kuwa hakuwa na "wasiwasi wowote" unaoashiria
kupendelewa kwa maslahi ya upande wowote wanchi za Atlantiki.
Alitaka Ulaya na Marekani ziwiane katika
kushughulika na Urusi na China, suala ambalo alisema linaweza kuwa kgumu
ukizangatia China ni mshindani na mshirika muhimu kwa Magharibi.
"Katika miaka ya hivi karibuni, China
imepata nguvu ya ulimwengu, na sisi kama washirika na wanademokrasia, lazima
tufanye kitu kukabiliana na hii," Bi Merkel alisema, akisisitiza ahadi za
Ujerumani na Marekani katika kusambaza chanjo katika nchi zinazoendelea ambapo
amesema nchi yake itaongeza Euro bilioni 1.5.
4. Kiongozi wa Ufaransa anasema ushawishi wa Marekani duniani unapaswa kukubaliana na hali halisi
Akiongea kwa katika video baada ya Rais Biden
kuhutubia ujumbe wa "Marekani imerudi" kwa mkutano huo, Bwana Macron aliweka
wazi kuwa Marekani sasa inapaswa ikubaliane na ukweli kwamba ile dhana ya kutawala
Ulimwengu sasa imepitwa na wakati na Ulaya inapaswa "kujisimamia zaidi
katika usalama wake."
Kwa vitendo, itachukua miaka mingi kwa Ulaya
kuimalisha jeshi la ulinzi ambalo litafanya Marekani iweze kujitegemea zaidi.
Lakini Bwana Macron ameazimia kuanza sasa akiwa ameazimia kuongeza uwezo wa
kiteknolojia wa Jumuiya ya Ulaya ili ipunguze kutegemea Marekani au China.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia
amesisitiza umuhimu wa nchi masikini kupatiwa chanjo na kwa ajili hiyo
amependekeza kwa Umaoja wa Ulaya na Marekani, mpango wa kupeleka dozi milioni
13 barani Afrika ili kwanza kuwapatia chanjo wahudumu wa afya wapatao milioni
milioni 6.5.
5. Marekani inajiunga rasmi na makubaliano ya hali ya hewa ya Paris
Makubaliano hayo ya kimataifa yaliundwa kuzuia
janga la joto duniani. Rais Biden amesema kukabiliana na shida ya hali ya hewa
ni miongoni mwa vipaumbele vyake vya juu na alitia saini mkataba saa chache tu
baada ya kuapishwa katika ofisi mwezi uliopita.
"Hatuwezi kuchelewesha tena au kupuuza
kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa," Bwana Biden alisema. "Huu
ni mgogoro wa ulimwengu, uliopo. Na sote tutapata matokeo ikiwa tutashindwa.
"
6. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen anataka Marekani ijiunge na juhudi za kuratibu makampuni makubwa ya mtandao
Kuratibu nguvu za kampuni kubwa za teknolojia
itakuwa "hatua muhimu" katika kukomesha vurugu za kisiasa,
alisisitiza, akiongeza: "Tunataka muongozo ulio wazi kwamba makampuni ya
mtandao yanawajibika kwa maudhui yanayosambazwa, na wanayounga mkono."
Maamuzi juu ya maudhui hayapaswi kuachwa kwa
“programu za kompyuta”. alisema. Lazima zifanywe na wabunge waliochaguliwa
kidemokrasia, hoja ambayo Ufaransa imekuwa ikitoa mara kwa mara.
Katika kuunga mkono juhudi za kusaidia nchi
zinazoendelea katika kusambaziwa chanjo,Kwa upande wake Bi. von der Leyen
alisema Halmashauri ya Umoja wa Ulaya nayo itaongeza mchango wake kutoka Euro
milioni 500 hadi Euro bilioni 1.5.
7. Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni aonya kuhusu
athari za usambazaji wa chanjo usio na uwiano
Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi
mkuu wa WHO, Ijumaa alihimiza nchi na watengenezaji wa dawa kusaidia
kuharakisha utengenezaji na usambazaji wa chanjo kote ulimwenguni, akionya kuwa
ulimwengu unaweza kupata athari kubwa ikiwa nchi zingine zitaendelea na kampeni
zao za kujilimbikizia chanjo na kuwaacha wengine nyuma.
"Usawa katika chanjo sio kitu sahihi tu,
lakini pia ni busara zaidi kufanya," Dk Tedros alisema katika Mkutano wa
Usalama uliofanika Munich, akisema kwamba kadri inavyochukua muda mrefu kutoa
chanjo kwa watu katika kila nchi, ndivyo janga hilo litakaa kinyume na
udhibiti.
Nchi tajiri zimekuwa zikikosolewa kwa wingi katika
wiki za hivi karibuni juu ya kujilimbikizia chanjo na kusahau nchi zenye kipato
cha chini na cha kati.
G7, ambayo inaundwa na Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japani, Amerika, na EU, ndio jukwaa pekee ambalo jamii zenye ushawishi mkubwa ulimwenguni na uchumi wa hali ya juu huletwa pamoja kwa mazungumzo ya karibu.
Matarajio ya Johnson ni kutumia G7 kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama. Kwa kuzingatia hilo, Bw.Johnson alialika viongozi kutoka Australia, India, na Korea Kusini kuhudhuria kama wageni ili kukuza utaalam na uzoefu.
Mataifa haya, pamoja na yale katika G7, yanawakilisha watu bilioni 2.2 na zaidi ya nusu ya uchumi wa ulimwengu. Makubaliano ya usalama kati yao yatakuwa na athari kubwa zaidi ulimwenguni, kuonyesha jinsi mataifa yanavyoshirikiana kuwafanya raia wao kuwa salama na wenye mafanikio zaidi.
Leave a comment