Habari

Sintofahamu Yaibuka Baada ya Namungo FC Kushikiliwa Angola

Msafara wa Namungo FC umekwama uwanjani hapo kwa madai ya baadhi ya wachezaji kupimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona

Mapema leo, iliripotiwa kuwa Namungo FC ilizuiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luanda nchini Angola ikidaiwa baadhi ya wachezaji wamekutwa na Virusi vya Corona.

Namungo FC imekumbana na sintofahamu hiyo baada ya kutua katika uwanja wa ndege nchini Angola kwa ajili ya mchezo unaofanyika kesho Februari 14, 2021 dhidi ya Primeiro De Agosto

Msafara wa Namungo FC umekwama uwanjani hapo kwa madai ya baadhi ya wachezaji kupimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amelielezea tukio hilo kuwa ni Siasa za Kimichezo na kusema, "Sisi kama Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje tunalifanyia kazi jambo hilo ili Timu hiyo iweze kushiriki michezo na kurudi nyumbani"
Aidha, Mkurugenzi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Tanzania Yusuph Singo pia ametoa tamko akisema wanajitahidi kwa ukaribu kuwasiliana na ubalozi wa Tanzania Nchini humo ili kulitatua suala hilo.
"Hatuko kimya na sisi kama Serikali tumeshituka na kushangazwa na hilo lakini tunalifanyia kazi tunawasiliana na wenzetu walioko huko," amesema.

Wachezaji wa Timu ya Namungo waliondoka nchini hapo jana wakielekea nchini Angola kwa ajili ya mchezo unaofanyika kesho, Februari 14, 2021.