Afrika

Simba yaitungua AS Vita nyumbani kwao Kinshasa

Ushindi wa Simba unawaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba wamewatoa kimasomaso mashabiki wake baada ya kuibuka washindi katika mchezo wa kwanza wa kundi A Michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Katika mchezo uliochezwa usiku wa Ijumaa Februari 12 katika dimba la Mashahidi jijini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Simba wamewashangaza wenyeji kwa kabumbu safi na hatimaye kuzoa alama zote tatu muhimu baada ya kushinda kwa goli moja kwa mkwaju wa penati.

 

Simba walipata mkwaju wa penati dakika ya 60 ya mchezo kufuatia shambulizi la nguvu walilofanya katika lango la wenyeji wao AS Vita. Mshambuliaji Chris Mugalu aliwaibua wanamsimbazi kidedea baada ya kupachika mkwaju huo nyavuni na kuwapa goli pekee la mchezo huo. Simba ambao wamepangwa katika moja ya kundi gumu zaidi la michuano watatupa karata yao ya pili na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri mnamo Februari 23 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Ushindi wa Simba unawaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika hatua ambayo si ngeni kwao kwani wameshacheza mara nne katika hatua hiyo na zote wakishindwa kufika nusu fainali.