Habari

Serikali Yafutilia Mbali Waraka wa Prof. Bisanda Kuhusu Tahadhari ya Corona

Tamko kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia limedai kuwa waraka wa tahadhari ya #COVID19 uliotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria ni batili

Wizara ya Elimu imewataka Wanafunzi na Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Huria kuendelea na masomo na kazi kama kawaida tamko ambalo limetolewa na wizara baada ya ushauri uliotolewa na  makamu mkuu wa chuo hicho Prof. Elifas Bisanda ukitaka mikutano na masomo yafanyike kwa njia ya mtandao ikiwa  moja kati ya tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Tamko kutoka Wizara ya Elimu, sayansi na teknolojia limedai kuwa waraka wa tahadhari ya #COVID19 uliotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho ni batili.

“Maelekezo yaliyotolewa na Prof. Bisanda ambayo ni maoni yake binafsi hayajazingatia muongozo wa udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika shule, vyuo na taasisi za elimu nchini wa wizara ya afya wa terehe 27 mei 2020” inasema taarifa hiyo ya wizara ya Elimu.

Aidha, Wizara hiyo pia imetoa rai kwa Taasisi za Elimu kuzingatia maelekezo ya Serikali kuhusu udhibiti wa maambukizi ya Ugonjwa huo.

Kwenye Waraka wa Prof. Bisanda, Wanafunzi wanaoingia katika Chuo hicho walisisitizwa kukaa nyumbani na kusoma kwa mtandao. Pia, tahadhari ilitolewa kwa wanaokusudia kusafiri nchi za nje ikielezwa siyo salama sana  huku wafanyakazi wakiaswa kuendesha mikutano yao kwa njia ya mtandao.

Wizara ya afya nchini Tanzania bado haijathibitisha taarifa za uwepo wa wagonjwa au vifo vinavyotokana na virusi vya corona huku Aprili mwaka jana ikiwa ni mara ya mwisho kutolewa kwa taarifa za mwenendo wa maambukizi ya gonjwa hilo.