
Serikali nchini Tanzania imetangaza kuanza kutumia ndege
kunyunyizia dawa makundi ya nzige yaliyovamia wilaya ya Longido na Simanjiro
wakitokea nchini Kenya.
Taarifa za kuingia kwa makundi hayo zilitolewa kwa mara ya
kwanza siku ya Ijumaa na mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaibambe ambaye amesema
ndege ya Shirika la Chakula Duniani FAO inayotokea Nairobi inatarajia kuanza
kazi ya kunyunyuzia dawa leo.
“Kuanzia kesho
(22.02.2021) ndege maalum itaanza kazi kupulizia sumu kuua nzige waliovamia
maeneo ya Longido na Simanjiro ili wasiendelee kusambaa na kusababisha maafa”
alisema Waziri wa KIlimo, Prof. Mkenda
Waziri Mkenda amesema tayari wataalam wa Taasisi ya
Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) wapo wilayani Longido na Simanjiro wakiongozwa na
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake Dkt. Efrem Njau kwa kazi ya kudhibiti wadudu hao
waharibifu wa mazao ya kilimo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutookota wala kula nzige
watakaokuwa wameuwawa na viuatilifu (sumu) kwenye maeneo yote ambapo ndege hiyo
itapita kuua nzige kwani viuatilifu hivyo vinaweza kuwa na madhara kwa
binadamu.
Pia, ameagiza wataalam wa kilimo na watendaji wa vijiji
na kata kutoa taarifa kwa wananchi juu ya uwepo wa kazi ya kuua nzige hivyo
wasiwe na hofu watakapoona ndege inaruka chini kwenye maeneo.
“Wananchi wakiona nzige wameanguka chini wamekufa
wasiwachukue au kula kwa kuwa wengi watakuwa wamekufa kwa sumu” alisisitiza
Prof. Mkenda
Waziri huyo wa kilimo amesisitiza kuwa serikali
itahakikisha mazao ya wakulima na malisho ya mifugo hayaharibiwi na nzige ndio
maana ametembelea eneo hilo la Longido ambapo amebainisha mafanikio ya
kuwadhibiti tangu walipoingia nchini mwezi Januari mwaka huu kwenye baadhi ya
maeneo.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna na madhara yoyote yaliyoripotiwa
kusababishwa na nzige hao kwani eneo lililovamiwa kwa kiasi kikubwa ni pori
lakini pia asilimia kubwa ya nzige hao bado ni wadogo.
Mwaka jana makundi makubwa ya nzige yalivamia maeneo kadhaa nchini Kenya na Ethiopia na kuibua hofu ya kutokea kwa baa la njaa kutokana uharibifu mkubwa walioufanya.
Leave a comment