
Serikali imesema
kuwa haitatoa takwimu za maambukizi ya virusi vya corona kwani kufanya
hivyo ni kuongeza hofu kwa wananchi hali itakayopunguza kinga za miili yao na
kupelekea kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa
huo
Akizungumza na waandishi wa habari Naibu waziri wa Afya, Dkt.
Godwin Mollel amesema kuwa matumizi ya data za magonjwa yote ni kwa ajili ya
kuchakata na kisha kuja na mbinu za kisayansi kukabiliana na magonjwa hayo
lakini sio swala la kutaka kila wiki Waziri wa Afya aelezale waliofariki na
wagonjwa, kwani kufanya hivyo ni kuwatisha wananchi.
“Wanasema Tanzania haitoi data, matumizi ya data za magonjwa
yote, ni kwa ajili ya kuchakata na kisha kuja na mbinu za kisayansi kukabiliana
na magonjwa hayo lakini sio swala la kutaka kila siku Waziri wa Afya aelezale
kwenye TV waliofariki, wagonjwa, waliozikwa ni ujinga mtupu, unatishia taifa na
kufanya lisitulie,” amesema Dk. Mollel.
Katika hatua nyingine Dkt Mollel amewataka Watanzania kuondoa
hofu dhidi ya Virusi vya corona kwani hata nchi zilizochukua hatua kubwa za
kupambana na virusi hivyo ndizo zimeonekana kuwa na idadi kubwa ya maambukizi.
“Hivi ni nchi gani inaweza kuchukua hatua zaidi na bora za
kujikinga zaidi ya Marekani, Uingereza, au nchi zilizoendelea. Leo
tunavyozungumza hivi kati ya Marekani na sisi, ni wapi wameumia zaidi na
ugonjwa wa COVID-1?” amehoji Dkt Mollel.
Kauli hii imekuja wakati ambapo shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa
likitoa wito kwa mamlaka nchini. kuanza kutoa takwimu za watu waliambukizwa
ugonjwa wa COVID-19, kuhimiza matumizi ya njia za tahadhari zinazotolewa na
shirika hilo pamoja na kujiandaa kupokea chanjo dhidi ya COVID 19.
Katika taarifa yake ya February 20 mwaka huu, kuhusu
mwenendo wa COVID-19 nchini Tanzania, shirika la Afya Duniani (WHO)
lilielelezea wasi wasiwasi wake kuhusu idadi ya wasafiri wa Tanzania
waliopatikana na kuwa na virusi vya corona
Hata hivyo serikali imekuwa ikihimiza zaidi watu kuendelea
kuchukua tahadhari zinazotolewa na wizara ya Afya nchini dhidi ya maambukizi ya
Virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kumuomba Mungu na kutumia tiba asili.
Leave a comment