Habari

Serikali: Hatuna Fedha ya Kutengeneza Barabara ya Tanga - Morogoro

Kutokana na ufinyu wa bajeti kwa sasa Serikali haijapata fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekiri kukosa Fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara ya kutoka Tanga mpaka Morogoro kwa kiwango cha Lami.

Hayo yameelezwa leo April 6, 2021 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Msongwe Kasekenya.

Akijibu swali la Mbunge wa Kilindi, Omary Kigua aliyeuliza ni lini Serikali itajenga Barabara hiyo kwa kiwango cha Lami, Kasekenya amesema “Kutokana na ufinyu wa bajeti kwa sasa Serikali haijapata fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.”

Aidha, Kasekenya ameeahidi kuwa barabara hiyo ya kutoka Kilindi jijini Tanga mpaka Gairo mkoani Morogoro yenye urefu wa kilomita 115.7 itaendelea kufanyiwa matengenezo mara kwa mara ili iweze kupitika kwa vipindi vyote vya mwaka.