Habari

Rais Mwinyi Aungana na Wazanzibari Kumuaga Maalim Seif, Zitto Akosa Maneno

Maalim Seif Sharif Hamad ametajwa kuwa na misimamo ya kutaka utu au haki ya mtu isipotee

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi leo amewaongoza waombolezaji wakiwemo viongozi na wananchi kwenye mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

Mazishi ya Maalim Seif ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo yamefanyika kijijini kwake Mtambwe katika wilaya ya Wete visiwani Pemba

Kabla ya mazishi hayo, mwili wa marehemu maalim Seif uliswalia kwenye uwanja wa Gombani na kabla ya hapo pia katika msikiti wa Maamur jijini Dar es salaam pamoja na viwanja vya Mnazi Mmoja mjini Unguja.

Katika mahali ambapo mwili huo ulipita, maelefu ya waombolezaji walijipanga barabarani na kwenye viwanja ambavyo kulikuwa na swala ili kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo ambaye ametajwa kama nguzo muhimu ya umoja na mshikamano wa kitaifa. 

Akitoa salamu za chama, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe, amesema maalim Seif aliyaishi yale yote aliyoamini na kuwaasa viongozi wengine na vijana kuiga mfano wake na kuahidi kwamba chama cha Act kitayatimiza maono yake na kutoa ushirikiano unaohitajika kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

“Wengi mnafahamu kwamba mimi si mtu wa kukosa maneno, lakini leo nakosa maneno ya kumwelezea Mwenyekiti wangu Maalim Seif Sharif Hamad - nakosa maneno kwasababu Maalim mwenyewe ni maneno,” amesema Zitto.

Chama cha ACT Wazalendo kitakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa kinampata Mrithi Maalim Seif ndani ya kipindi wiki mbili.

Wengi mnafahamu kwamba mimi si mtu wa kukosa maneno, lakini leo nakosa maneno ya kumwelezea Mwenyekiti wangu, nakosa maneno kwasababu Maalim mwenyewe ni maneno
- Zitto Kabwe

Faraj Faridhi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambapo anasema kuwa kuna ugumu wa kuliziba pengo la Maalim Seif katika siasa za upinzani kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuthamini utu na haki za watu. 

“Maalim Seif Sharif Hamad ikumbukwe alikua na misimamo ya kutaka utu wa mtu usipotee au haki ya mtu isipotee, lakini katika siasa za Zanzibar, tumeona tangu mwaka 1995 kwa chaguzi zote mpaka 2020 kulikua hakuna mgombea wa upinzani mwenye nguvu wa kumfikia Maalim Seif na pia ikumbukwe siasa za Zanzibar ni mtu na mtu mwenyewe ni Maalim Seif Sharif Hamad,” amesema Faridhi

Maalim Seif amefariki dunia Februari 17 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa tangu Februari 9 kwa matibabu.