Habari

Rais Magufuli Amuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Zepharine Galeba

Jaji Zephrine Galeba alipandishwa cheo na Rais John Magufuli Februari Mosi, 2021 na kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa akiachana na nafasi yake ya awali ambapo alitumikia nafasi ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amuapisha Mhe. Jaji zepharine Galeba Kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania katika hafla ilyofanyika jijini Dodoma februali 2, 2021.

Jaji Zephrine Galeba alipandishwa cheo na Rais John Magufuli Februari Mosi, 2021 na kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa akiachana na nafasi yake ya awali ambapo alitumikia nafasi ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma. Uteuzi huo ulifanyika katika maadhimisho ya miaka 100 ya mahakama nchini yaliyofanyika mkoani Dodoma. 

Utoaji hukumu kwa lugha ya kiswahili katika kesi Na. 23 ya mwaka 2020 ya North Mara Gold Mine LTD dhidi ya Gerald Nzumbi, ulichangia kwa kiasi kikubwa uteuzi wa Jaji Zephrine Galeba na ilijidhihirisha zaidi katika kauli ya Rais Magufuli iliyosema “…Huyu [Jaji Galeba] ni shujaa wa Kiswahili katika [mhimili wa] Mahakama…unajua na ninyi mahakamani mko ‘very rigid’ (ni wagumu sana kubadilika)…kwa sababu ameamua kuenzi lugha ya Kiswahili, mimi leo ninampandisha cheo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Anakuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa kwa uzalendo huo, wa Kitanzania, wa kukwepa miiko iliyomo ndani ya Mahakama na kuandika hukumu kwa Kiswahili”.

Aidha, Baada ya kumuapisha Jaji Galeba, Rais Magufuli ameendelea kutoa wito kwa mahakama kuzingatia matumizi ya lugha ya Kiswahili Mahakamani na katika mifumo ya kisheria akiongeza kuwa  “Kiingereza kinaendelea kutumika Mahakamani na moja ya sababu inayotolewa ni kwamba Kiswahili hakina misamiati ya kutosha, kwangu Mimi sababu hii sina uhakika kama ina ukweli, Kiswahili ni lugha kubwa yenye Misamiati ya kutosha ndio maana kinatumika kwenye Taasisi za Kimataifa mfano AU, EAC,SADC na Vyombo Vya Habari maarufu Duniani TBC, BBC, DW, VOA nk”.

“Kusema Kiswahili hakina misamiati ya kutosha sio sahihi, lakini hata kama kwa mfano ingekuwa ni kweli Kiswahili hakina misamiati ya kutosha, nani anaweza kunitajia lugha inayojitosheleza kwa misamiati? haipo, ni wazi hatutumii Kiswahili kwa kukosa utashi na ujasiri”-JPM Alifafanua.