
Rais Dkt John Magufuli amewaongoza viongozi mbalimbali
na wananchi kuaga mwili wa Katibu Mkuu Kiongozi balozi John Kijazi
Shughuli za ibada na kuaga mwili huo zimefanyika
kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali akiwemo rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa
Rais.
Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Rais Magufuli
amesema marehemu Balozi Kijazi alikuwa mchapakazi aliyeipenda kwa dhati nchi
yake na alikuwa anaheshimu kila mtu bila kujali umri au cheo chake.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewataka Watanzania
wasitishike na ugonjwa wa corona na badala yake waendelee kuchukua tahadhari na
kumwomba Mungu.
"Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo Magonjwa ya
vifua ya kupumua na kadhalika yatakuwepo hayakuanzia hapa zipo nchi zimepoteza
watu wake wengi sisi Tanzania Mungu ametusaidia sana katika kipindi cha mwaka
uliopita," amesema Magufuli.
Amesema ugonjwa wa corona unaweza kuepukika kwa
kuchukua tahadhari na kumwomba Mungu na kuwaomba viongozi wa dini zote kuandaa
maombi kwa ajili ya janga hilo na kusisitiza kuwa nchi ya Tanzania haita chukua
hatua za kuwafungia watu wake ndani yaani Lockdown kwasababu ya virusi hivyo.
SOMA:
- Mfahamu
Marehemu Balozi Kijazi
Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kukemea uenezaji wa
taarifa za uongo kuhusu corona ikiwemo ile iliyodai kuwa waziri wa Fedha Dkt
Philip Mpango amefariki dunia kwa maradhi ya corona.
“Leo nimetumiwa ujumbe na waziri wa fedha Dkt Mpango
ambaye amelazwa Dodoma na ninaomba noisome hapa kwa faida ya wale waliokuwa
wanatweet Amenitumia leo asubuhi, ameniambia ‘Mheshimiwa Rais, asante sana
nimepata ujumbe wako kupitia kwa mke wangu, kwa neema ya Mungu naendelea
vizuri, ninakula, ninafanya mazoezi ya kifua na kutembea. Hao wanaonizushia
kifo kwenye mitandao niliwaombea msamaha kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana.
Mheshimiwa Rais, Mungu akubariki na akupe neema na ujasiri zaidi, katika
kuliongoza taifa letu katika wimbi hili. Naungana nawe na familia katika
maombolezo ya kifo cha mpendwa wetu, Mhe. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John
Kijazi. Rest In Peace.
Waziri Mpango’
Ni huyo ambaye aliambiwa jana amekufa,” alisema Rais
Magufuli.
Mazishi ya Balozi Kijazi ambaye amefariki usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma, yanatarajia kufanyika Februari 20 wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Leave a comment