
Kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Dkt. John Pombe Magufuli kilipokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa Watanzania na watu wa mataifa mbalimbali. Kabla ya taarifa rasmi ya kifo chake uvumi ulienea mitandaoni kuhusu afya ya hayati Magufuli. Uvumi huu ulizua hofu kwa waliompenda Magufuli na aina yake ya uongozi.
Baada ya sintofahamu kwa takribani wiki nzima, katika hali ambayo haikutarajiwa usiku wa Machi 17, 2021 aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye sasa ni Rais, Samia Suluhu Hassan alitangaza taarifa za kifo cha Rais Magufuli. Taarifa hizi ziliibua upya hisia za majonzi na fikra za mustakabali wa nchi. Kila mtu aliguswa kwa namna yake na kila mmoja alifanya alichoweza kuonesha namna alivyoguswa.
Vyombo vya habari vilifanya msiba huo kuwa ajenda kubwa ya kitaifa kwa kuhakikisha wanazungumzia msiba huo pekee kwa muda wote wa maombolezo na hata baada ya hayati Magufuli kupumzishwa katika nyumba yake ya milele. Wanasiasa, wanadiplomasia, wananchi wa kawaida, wasanii, viongozi wa dini na kila kundi kwa namna lilivyoguswa walimimina salamu za rambirambi kwa familia, serikali na Watanzania wote.
Viongozi mbalimbali wa Afrika na dunia walitoa salamu kwa kushiriki moja kwa moja, kupitia barua, mitandao na hata kusaini kitabu cha maombolezo. Watanzania wachache walipata nafasi ya kumuaga moja kwa moja jijini Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na hatimaye Chato ambapo alipumzishwa katika nyumba yake ya milele mnamo Machi 26, 2021.
Kwa upekee wanamuziki walishiriki shughuli za kuaga mwili kwa namna mbalimbali lakini kwa namna kubwa ya kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali za maombolezo. Wasanii wengi ambao wamekuwa karibu na serikali na kushiriki katika shughuli za kisiasa hasa wakati wa kampeni za kisiasa na wakati wa hafla mbalimbali za kiserikali waliingia studio na kuonesha hisia zao kufuatia kifo cha Magufuli.
Wizara ya Burudani hapa Serengeti Bytes imesikiliza na kuchambua nyimbo mbalimbali zilizotungwa kumsindikiza hayati Magufuli. Nyimbo nyingi zimesifia mambo aliyoyafanya wakati wa uongozi wake na kugusia namna ambavyo ameiacha nchi katika hatua nzuri ya maendeleo. Wanamuziki wengi wamesisitiza mambo ambayo tayari yamechambuliwa na wachambuzi wengi ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, huduma za afya, maji na kadhalika.
Wasanii pia wameeleza kuondoka kwa Magufuli kwamba imeacha pengo lisilozibika. Mambo mengi yaliyowasilishwa na wasanii kupitia nyimbo za maombolezo yanaweza kupingwa kupitia mijadala huru, lakini ni mawazo yao na sisi tumeyaweka hapa kama yalivyo.
Tumekuwekea hapa orodha ya nyimbo 20 bora zaidi wakati wa maombolezo ya kifo cha Magufuli.
20. Magufuli - Jux
19. Ndivyo Ulivyo – Tanzania Gospel Artists
18. Nenda Shujaa - Barnaba
17. Lala Salama – Linex ft Dkt. Elizabeth Kilili & Angel Voice
16. Baba Akupokee – Ommy Dimpoz ft Mwana FA
15. Mzalendo – Wanyabi ft Vasmo
14. Safiri Salama – Bahati
13. Wosia – Kala Jeremiah ft One Six
12. Tutaonana Magufuli – Peter Msechu
11. Tutakukumbuka Daima – Christina Shusho
10 Wosia wa Magufuli – Alikiba
09. Nenda Salama Magufuli – Whozu & Odong & Baddest 47
08. Bye Magufuli – Aslay
07. Ahsante Magufuli – Konde Music Artists
06. Kifo – Rayvanny
05. Tutabaki Nawe – Tanzania All Stars (Clouds Media)
04. Umetuacha Imara – Peter Msechu
03. Lala Salama – Tanzania All Stars (Wasafi Media)
02. Hayasahauliki – Tanzania Icons
01. Kwa Heri Rais Magufuli – Goodluck Gozbert
Sikiliza kisha toa maoni yako. Apumzike kwa Amani hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Leave a comment