Tanzania

Ni kwa Namna Gani Sampuli za Bure Huishia Kugharimu Pesa Yako?

Ingawa kawaida tunafahamu kuwa sampuli za bure ni ujanja wa mauzo mara nyingi bado tunaangukia kwenye mtego wa huo na kujikuta tukitumia pesa kufanya manunuzi

Fikiria siku ambazo ulikuwa unazunguka tu kwenye maduka makubwa ili uone duka gani siku hiyo linagawa sampuli za bidhaa zao bure. Sampuli za bure ziko kila mahali na hakika hutamanisha na zina uwezo wa kuchangamsha siku yako kama utabahatika kuipata.

KWANINI WAFANYABIASHARA HUTOA BIDHAA ZA BURE?

Inafurahisha sana kupata bidhaa bila kutumia pesa yoyote. Lakini inafanyaje kazi kwa wauzaji?

Kugawa bure kiasi kidogo cha bidhaa wanazouza kawaida husaidia kuongeza mauzo yao kwa kiasi kikubwa kwa wauzaji wengi. Kutoka kwa mtazamo wa kibiashara, kuruhusu watu kujaribu bidhaa bila malipo ina faida nyingi kwa sababu:

  • Kutangaza uwepo wa bidhaa mpya
  • Kuiweka biashara midomoni mwa watu ili biashara iwafikie watu wengi
  • Kupata mrejesho wa haraka ili ujue ni kwa namna gani unaweza kuboresha biashara yako.
  • Kupata mauzo mazuri ikiwa watu watapenda bidhaa yako

Je, Sampuli za Bure Huleta Matokeo Mazuri?

Uchunguzi wa kibiashara unathibitisha kuwa ugawaji wa bidhaa za bure ni silaha yenye nguvu na nzuri ya kukuza biashara. Sampuli za bure huboresha uaminifu wa wateja na mitazamo, sio kwa bidhaa tu, bali pia kampuni inayowapa.

Kwanini Bidhaa za Bure Huzaa Matunda Mazuri?

Akili ya binadamu ni rahisi sana kupumbazwa na vitu vidogo na ndio maana unaona vitu kama sampuli za bure zinatufanya tuingukie kwenye mtego wa ujanja wa mauzo.

Kwa hivyo hata ingawa kikawaida tunafahamu kuwa ni ujanja wa mauzo mara nyingi watu huangukia kwenye mtego wa huo na kujikuta wakitumia pesa yao kufanya manunuzi.

 

Ni Namna Gani Bidhaa za Bure Hucheza na Saikolojia Yako?


Haja ya Kurudisha Wema

Ishara yoyote inayoashiria fadhila moja hutufanya tutake kurudisha au kurudisha neema.

Kukubali kuchukua sampuli za bure kunaweza kukushawishi kununua pakiti kubwa zaidi ya bidhaa. Ingawa wakati mwingine unbaweza ukawa hujaipenda bidhaa lakini ukanunua ukihisi unarudisha fadhila.

Hukoleza Uaminifu

Tunapenda kupata vitu vya bure. Na kwa hivyo, tunapenda watu ambao hutupatia vitu vya bure. Kama watumiaji, tunataka kununua kutoka kwa watu ambao hufanya maisha yetu kuwa rahisi na ambao ni wema kwetu. Kwa hivyo tunapopokea bidhaa au huduma za bure, tunaanza kukuza uhusiano na muuzaji na kujitoa kununua kutoka kwao.

Kwa hivyo wakati mtu anatoa sampuli za bure, tunaanza kuwapenda mara moja; na kadri muda unavyokwenda husababisha kuwa waaminifu kwa wauzaji hawa. Hii inamaanisha, tunaweza kugeuka na kuwa wateja wa kudumu kama ikitokea tumependa bidhaa zao.

Hujenga Tamaa

Mara ngapi imekutokea kwamba haukuwa na nia ya kununua bidhaa fulani; lakini baada ya kujaribu sampuli, ukaamua kununua bidhaa hiyo?

Sampuli hushtua akili zetu na kutumbusha raha tunayoweza kupata kama tukinunua kiasi kikubwa cha bidhaa hiyo tofauti na uliyoonjeshwa.

Hukuondolea Wasiwasi

Watu wengi wanaogopa bidhaa mpya kwa sababu wana wasiwasi juu ya kutokupenda. Tuna wasiwasi itakuaje kama itatokea umenunua bidhaa halafu hujaridhika nayo; hiyo hutafsiriwa kama upotevu wa muda na pesa. Lakini kujaribu sampuli ya bure huondoa mashaka ambayo huweza kukukwamisha kufanya manunuzi.

Wakati kampeni ya ugawaji wa sampuli za bure inaweza ikawa na hatari kwa kampuni, kwao bado ni njia bora ya kukuza manunuzi na kuboresha bidhaa zao.