Habari

Namungo FC Yadai Wachezaji wake Kukutwa na Corona ni Uzushi, Wachezaji Walia Njaa

"Hatukupata chakula chochote tangu walipowasili Zaidi ya maji na matunda"

Klabu ya Namungo FC imekwama kwa  mara ya pili sasa kurejea nchini Tanzania kutokana na kuahirishwa kwa mchezo wake dhidi ya CD De Agosto kutoka katika mji wa Luanda  nchini Angola.

Taarifa za awali zilieleza kuwa timu hiyo ilipaswa kurejea nchini mapema Jumamosi Lakini mamlaka nchini Angola zilisitisha safari hiyo zikidai kuwa marubani wa ndege ya kukodi ambayo ilipaswa kuwasafirisha wachezaji hao walitakiwa wapumzike. 

Hata hivyo klabu hiyo kutoka kusini mwa Tanzania ilitarajiwa kuanza rasmi safari yake ya kurejea Dar es salaam mapema leo lakini safari hiyo imekabiliwa na mkwamo kutokana na watu watatu kukutwa na virusi vya corona na kuwekwa katika karantini nchini humo ambapo mamlaka zimewazuia watu hao kuondoka. 

Mwenyekiti wa timu hiyo, Hassan Zadidu amewataka Watanzania kuiombea kwani inakumbana na changamoto ambazo kwao ni ngumu kuzikabili kutokana na mazingira huku akidai kuwa suala la wachezaji wawili na afisa mmoja katika msafara huo kukutwa na virusi vya corona ni la uzushi

“Lakini kwa bahati mbaya sana kitu wanachotumia ni cha uongo wanasema wamewapima test ya kwanza wako positive lakini wanasema wamewapima test ya pili wako positive lakini tulipowauliza kwa njia ya simu wakasema hawajawapima kwa mara ya pili kwahiyo ni uongo tu na udanganyifu,” amesema Zadidu.

Baadhi ya wachezaji wamesema kuwa hawakupata chakula chochote tangu walipowasili zaidi ya maji na matunda huku wakidai kuwa wanateseka na kupitia katika mazingira magumu 

Shirikisho la soka Barani Afrika CUF liliahirisha mchezo wa kombe la Shirikisho baina ya timu hizo mbili uliopangwa uchezwe Jumapili ya tarehe 14 February mwaka huu, kutokana na msafara wa timu ya Namungo kutakiwa kukaa karantini kutokana na kadhia hiyo CAF Imesema kuwa italifikisha suala hilo kwenye kamati husika kwa ajili ya uamuzi. 

Klabu ya Namungo iliingia katika hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho baada ya ushindi wa Agregate ya 5-3 dhidi ya Al-Hilal-Obeyed baada ya timu hiyo kushindwa kucheza mchezo wake wa marudiano wakati CD De Agosto ya Angola ikifikia hatua hiyo baada ya kufungwa goli moja kwa bila dhidi ya Kaizer Chiefs kwenye mchezo wakufuzu hatua ya makundi ya klabu bingwa barani Afrika 

Nchi ya Angola ni miongoni mwa mataifa ambayo  yanatekeleza makatazo na tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona amabapo kufikia February 10 nchi hiyo imeripoti visa 3262 vya Covid 19 na watu 57 na mpaka sasa  wamefariki nchini humo.