Habari

Mume wa Malkia Elizabeth wa Uingereza Afariki

Mwanamfalme Philip, mume wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 99, Kasri la Buckingham limetangaza.

Nchi ya Uingereza imepata pigo la kuondokewa na Mwanamfalme Philip aliyejulikana kama Mtawala wa Edinburgh na aliyekuwa Mume wa Malkia Elizabeth II.Mwanamfalme Philip amefariki kwa maradhi ya moyo akiwa na Umri wa Miaka 99 katika Jumba la kifalme la Windsor lililopo Magharibi mwa London.

Kasri la kifalme kwa kupitia Mtandao wake wa Twitter limetangaza Leo Ijumaa Tarehe 09/04/2021 kuwa " Ni kwa Masikitiko Makubwa, Mtukufu malkia anatangaza Kifo cha Mumewe Mpendwa, Mwanamfalme Prince Philip Mtawala wa Edinburgh, Mwanamfalme amefariki leo asubuhi katika Jumba la Windsor, Familia ya kifalme inaungana na watu wote duniani kuomboleza Msiba huu.”

Mwanamfalme Philip Kipindi cha Uhai wake Alikuwa upande wa Malkia katika Kipindi chote cha Utawala wake wa Miaka 69, ambao ni muda mrefu zaidi katika historia ya Uingereza.

Wanandoa hao walioowana mnamo mwaka 1947, Miaka Mitano kabla ya Malkia Elizabeth II kurithi kiti cha ufalme wa Uingereza.

Aidha, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ametoa pole kwa familia ya kifalme na kwa wananchi wote wa Uingereza huku akimsifu akisema enzi za uhai wake, mwanamfalme atakumbukwa “kwa Msaada wake thabiti kwa Malkia, sio tu kama mke wake, bali kukaa kando yake kila siku ya utawala wake, kama mumewe, akimtia nguvu na kukaa kwao kwa zaidi ya miaka 70."

Mtawala wa Edinburgh kama alivyojulikana mapema mwaka huu alilazwa hospitalini kwa wiki 4 mfululizo akipatiwa Matibabu ya moyo na mapema mwezi wa 3 mwaka huu aliruhusiwa.

Mara ya mwisho Mwanamfalme Philip kuonekana kwenye umati ilikuwa ni Julai mwaka jana kwenye hafla ya kijeshi katika Jumba la Windsor, Ikulu ya Kifalme Magharibi mwa Jiji la London.