Habari

Mrithi Arithishwa Othman Sharif Aapishwa Kumrithi Maalim Seif

“Ninao uzoefu, nchi hii inastahili kwenda mbele sijawahi kuwa na historia ya kushindwa

           

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt Hussein Mwinyi amemuapisha Othman Masoud Sharif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kuchukua nafasi Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki Februari 17, 2021.

Akizungumza baada ya kuapishwa Othman amesema kuwa kazi yake kubwa ni kuendelea kujenga misingi iliyoanzishwa na Dk Mwinyi na Maalim Seif akisisitiza kuwa hana historia ya kushindwa jambo.

“Ninao uzoefu, nchi hii inastahili kwenda mbele sijawahi kuwa na historia ya kushindwa kwa hiyo nakwenda kusimamia misingi yote iliyoanzishwa,” amesema Othman.

Katika hatua nyingine Ameitaja baadhi ya misingi hiyo kuwa ni uwajibikaji, utengenezaji wa sera bora za kuleta maendeleo, kusimamia ustawi wa jamii ya Wazanzibar, uchumi, maridhiano na kuleta amani na utulivu.

Lakini Othman Masoud Sharif ni Nani….?

Amewahi kuwa kwenye tume ya wanasheria  wa serikali mwaka 1989 mpaka mwaka 1993 pia amewahi kuwa katibu mkuu katika wizara ya nchini na masuala ya kisheria mwaka 1993 mpaka mwaka 1996 chini ya utawala la Rais wa awamu ya tano wa Zanzibar Salmin Amour

Amekuwa katibu   kupitia wizara mbalimbali, katika nyakati tofauti kuanzia mwaka 1996 mpaka mwaka 2002  akihudumu katika wizara za katiba na utawala bora, wizara ya nchi haki na masuala ya kikatiba.

Wakati wa Rais Amani Abeid Karume aliteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa mashtaka  wadhifa aliohudumu mpaka mwaka 2011 kabla ya kuwa kamishna wa Tume ya mipango ya Zanzibar kuanzia mwaka 2011 mpaka mwaka 2014

Pia Rais wa Zanzibar kwa wakati huo, Dkt Mohamed Shein alimteua kuwa  mwanasheria mkuu wa Zanzibar kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2014, akiwa pia mjumbe wa baraza la mawaziri na Mbunge wa bunge la wawakilishi kutoka Zanzibar.

 Othman Masoud Othman alishiriki kwa kiasi kikubwa katika kuandaa muswada wa marekebisho ya katiba ya Zanzibar. Marekebisho ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Akiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar chini ya utawala wa Dkt. Ali Mohammed Shein, alitofautiana na msimamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika baadhi ya vifungu vya rasimu hiyo. Hususani muundo wa Muungano unaopaswa kuwepo kati ya Zanzibar na Tanganyika. Othman Masoud hakukubaliana na muundo wa serikali mbili uliokuwa ukipigiwa debe na CCM na SMZ. Na badla yake Alisimamia muundo wa muungano wa serikali tatu.

Wadadisi wa mambo wanaamini msimamo huo ndio uliomtia katika kashikashi katika majengo ya Bunge. Na ulifikisha tamati wadhifa wake wa mwanasheria mkuu kwa kuenguliwa Oktoba 2014. Na hapo ndipo safari yake katika siasa za upinzani ilipoanza kupitia vyama vya CUF na ACT Wazalendo

Othumani Masoud Othumani ni Msomi wa masuala ya kisheria aliyezaliwa Pandani, Wete huko visiwani Pemba  mwaka  1963, Amepata elimu yake ya Juu ya  sheria katika vyuo vikuu mbalimbali ikiwa ni pamoja na  chuo kikuu cha Dar es salaam mwaka 1989, chuo kikuu cha Londoni Huko Uingereza pamoja na chuo kikuu cha TURIN Huko nchini Italy.