Habari

Motsepe Atayaweza Makandokando ya Soka la Afrika?

Ni mfanyabiashara, hivyo tunategemea kuwa atatumia mbinu mbadala kuisaidia CAF kupata Mapato

Bilionea wa Afrika Kusini, Patrice Motsepe, amechaguliwa bila kupingwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Kandanda barani Afrika, CAF, kwenye mkutano mkuu wa uliofanyika nchini Morocco.

Uchaguzi wake unafuatia makubaliano yaliyosimamiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Gianni Infantino, wiki moja iliyopita, ambayo yanawawezesha wapinzani watatu wa Motsepe kuteuliwa kushika nyadhifa za umakamu wa rais wa CAF.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kwake, Motsepe ametoa wito wa kufanya kazi pamoja ili kuupeleka mbele mchezo wa soka barani Afrika na ameahidi kurejesha mafanikio yaliyowahi kupatikana kwenye kandanda miaka iliyopita.

"Waafrika wanahitaji Busara za pamoja inahitaji watu wenye kujitoa na kufanya kazi katika kila taifa tunapofanya kazi kwa pamoja soka letu linakuwa na sote tunapata furaha ambayo tumeikosa huko nyuma" amesema Motsepe 

”Nadhani Motsepte atakuwa na kazi kubwa ya kufanya kurejesha hadhi ya CAF"
- Katende Malibu, Uganda

Baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya  michezo barani Afrika wanaona kuwa bado kuna uingiliwaji mkubwa wa maamuzi kutoka FIFA, katika chombo hicho chenye mamlaka makubwa yakisoka barani Afrika huku wengine wakitilia shaka upatikanaji wa Motsepte na kutengeneza hisia kwamba huenda akakabaliana na kizingiti kizito pale atakapohitaji kutimiza matakwa ya Waafrika yanayokinzana na Shirikisho la soka Duniani FIFA Kama anavyotueleza Gharib Mzinga mwandishi wa habari za michezo na mchambuzi wa masuala ya soka hapa nchini.

“Unaweza kujiuliza ni kwanini wamekubali kwasababu siasa za mpira zilivyo mara nyingi Rais wa shirikisho la soka Duniani FIFA Kama Infantino anaposhauri jambo basi inabidi mlifuate msipolifuata kuna vikwazo vingi sana mnaweza mkawekewa ndani yake na mkakosa hata baadhi ya nafasi nyingine” amesema Mzinga. 

Kwa Upande wake Fred Katende Malibu mwandishi wa habari za michezo kutoka nchini Uganda yeye anaamini kuwa Motsope atakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwaajili ya soka la Afrika na kurejesha hadhi ya shirikisho hilo. Malibu anasema kuwa ni ngumu kwa bara la Afrika kuzuia uingiliaji wa maslahi ya shirikisho la soka Duniani FIFA Kwa kuwa shirikisho hilo ndilo lenye maamuzi ya mwisho kwenye soka 

”Nadhani Motsepte atakuwa na kazi kubwa ya kufanya kurejesha hadhi ya CAF, Ni mfanyabiashara hivyo tunategemea kuwa atatumia mbinu mbadala kuisaidia CAF kupata Mapato kupitia Biashara, Haki za matangazo na wadhamini vilevile anapaswa kuongeza thamani ya mashindano ya CAF” amesema Malibu. 

Katika hatua nyingine Rais wa FIFA Gian Infantino amempongeza Motsepe kwa ushindi huo na kumtakia mafanikio kiongozi huyo, katika miaka yake minne ya uongozi akiwatakia heri pia viongozi wenzake wa CAF Pamoja na kuwapongeza viongozi wa awamu iliyopita kwa kazi walioifanya. 

Motsepe, ambaye ni mfanyabishara mwenye mafanikio makubwa asiye na uzoefu mkubwa katika kusimamia kandanda, atamrithi Ahmad Ahmad aliyechaguliwa kuingoza CAF miaka minne iliyopita, lakini akaondolewa kwa tuhuma za rushwa.