Habari

Meli Kubwa ya Mzigo Yaziba Mfereji wa Suez

Meli ya Ever Given ilikwama karibu na mwisho wa mfereji Jumanne baada ya kupoteza uelekeo kutokana na upepo mkali na dhoruba ya vumbi, Mamlaka ya Mfereji wa Suez ilisema

Moja ya meli kubwa ya mizigo inayofahamika kama Ever Given Marine imekwama  kwenye mfereji wa Suez na kusababisha msongamano wa meli katika moja wapo ya njia zenye shughuli za biashara ulimwenguni.

Mfereji wa Suez ni moja wapo ya njia muhimu za maji ulimwenguni na inaunganisha Bahari ya Shamu na njia za usafirishaji kwenda Asia. Ina urefu wa km190, mita 24 kwenda chini na mita 205 kwa upana na inaweza kushughulikia meli kadhaa kubwa za makontena kwa siku.

Ever Given iliyo na urefu wa mita 400 sawa na urefu wa viwanja vinne vya soka na upana wa mita 59 imeziba njia za meli zingine ambazo zimekwama pande zote.

Meli hiyo iliyo na ukubwa wa tani 200,000 iliundwa mwaka 2018 na ilikuwa ikiendeshwa na kampuni ya uchukuzi ya Taiwan, Evergreen Marine ilikwama majini siku ya Jumanne

Evergreen Marine, imesema meli hiyo "huenda ilikabiliwa ghafla na upepo mkali, ulioifanya kupoteza mkondo… na kwa bahati mbaya kugonga chini na kukwama"

Ever Given ilikwama karibu na mwisho wa mfereji Jumanne baada ya kupoteza uelekeo kutokana na upepo mkali na dhoruba ya vumbi, Mamlaka ya Mfereji wa Suez ilisema.

Misri imesema imefungua njia ya zamani kugeuza mkondo wa meli zingine ili kuzuia msongamano, huku kukiwa na wasi wasi njia ya sasa itazibwa kwa siku kadhaa.

Tukio hilo tayari limesababisha msongamano wa majini huku baadhi ya meli zikikosa njia ya kupita.

Boti kadhaa za kukokota zinafanya kazi ya kuikomboa meli hiyo iliyozuia njia huku Wataalamu wakihimiza umakini wakati wa oparesheni ya kuondoa Ever Given, ambayo inajumuisha kuondoa kiwango kikubwa cha mchanga iliyozunguka sehemu iliyokwama meli hiyo, huenda ikachukua siku kadhaa.

Tukio kama hilo limeshawahi kutokea hapo awali ambapo mnamo mwaka wa 2017, meli ya Japani ilikwama lakini ilirudishwa ndani ya masaa kadhaa. Mbali na mfereji huo, tukio kubwa zaidi lilitokea karibu na bandari ya Ujerumani ya Hamburg mnamo 2016 wakati Meli kubwa ya CSCL ilipokwama na kuhitaji maboti 12 kuikomboa zoezi lililochukua takribani siku tano.