Stori

Mauaji ya Waziri Mkuu mstaafu katikati ya ombwe la kisiasa Italia: Kuzaliwa na kufa kwa kundi la RED BRIGADE (Sehemu ya Pili)

Inatoka sehemu ya kwanza

Baada ya serikali kuonekana kutotia nguvu kumuokoa Moro kwa kutofanya makubaliano na kundi hilo, ni dhahiri maisha ya Moro yalikuwa hatarini. Kelele na msukumo wa watu kuiomba serikali kufanya nalo mazungumzo hazikusikilizwa. Hata kelele za Papa Paul VI za kuomba serikali ifanye mazungumzo na kundi hilo ili kunusuru maisha yake, hazikufua dafu.


Basi barua ya mwisho kutoka kwa Moro katika mfululizo wake wa barua, ilikwenda kwa mke wake, iliandikwa Mei 7. Ilikuwa barua ya kumuaga na dhahiri ikibeba simanzi na kukata tamaa: "Wameniambia kwamba si muda mrefu wataniua, nakubusu kwa mara ya mwisho", ilisema sehemu ya barua hiyo aliyoandikiwa mkewe kipenzi, Eleonora Chiavarelli, ambaye baadaye aliwapiga marufuku viongozi wa serikali na chama cha DC kuhudhuria mazishi ya mumewe kwa kudai walizembea makusudi kushughulikia uhai wake kwa kuwa walitaka afe. Kweli, siku mbili mbele, mwili wake ulikutwa umetelekezwa garini katikati ya viunga vya Rome, katika barabara ya Caetani, ukiwa umetobolewa kifuani kwa risasi.

Ndiyo, ushikiliwaji mateka wa kiongozi mkubwa wa nchi kwa siku 54, tena ndani ya nchi, na baadaye mauaji yake, ilikuwa ni kitendawili kwa nchi hiyo iliyokuwa tenge kiusalama wakati huo. Kitendawili kilichoacha maswali kuliko majibu, ya je, ni kweli kundi la Red Brigade ndilo lililomteka na kumuua? Na kama siyo, nani alikuwa nyuma yake? Ni nani hasa alitaka Moro afe ili kuinusuru Italia na mkwamo zaidi wa kisiasa? Kwanini Marekani, Uingereza, NATO, na serikali ya Italia hawakutia juhudi kumuokoa Moro kama walivyofanya miaka mitatu mbele, 1981 kwa Mmarekani aliyekuwa akihudumu NATO Italia, Jenerali James Lee Dozier aliyetekwa na kundi hilo na kuokolewa na kikosi maalumu cha NOCS cha Italia? Kwanini serikali ya Italia imeweza kutegua kitendawili kwa kufanya uchunguzi na kupata majibu kwa mashambulizi na wale wote waliotendewa ubaya na Red Brigade, lakini imeshindwa kwa kiongozi mzito kama Moro?

Basi katika kujibu kitendawili hiki cha mauaji ya Moro, kumeibuka nadharia nyingi kukihusu. Lakini mbili zimepata mashiko kiasi chake. Nadharia ya kwanza inayosema mauaji ya Moro yana mkono wa mataifa ya nje yenye nguvu yaliyovutana kiitikadi (lucidi superpowers) - Marekani na Umoja wa Kisovieti sanjari na mashirika yao ya kijasusi ya CIA na KGB, au na askari wa siri wa NATO wa "Operation Gladio". Mtu wa kwanza kuiongelea nadharia hii, ni mwandishi nguli wa habari za uchunguzi na upelelezi- juu ya siasa, uhalifu na makundi ya uhalifu - Mino Pecorell, aliyekuwa akiandika katika gazeti la "Osservatore Politico".

Mara baada ya utekaji na mauaji ya Moro, mwaka uliofuata, Mei 1978, Pecorelli aliandika katika gazeti lake la "Osservatore Politico" juu ya nadharia hii ambayo alidai kuhusika kwa mataifa yenye nguvu(lucid suoerpowers) kwa madhumuni ya kulinda kile alichokiita misingi ya mkutano wa Yalta 1945(Logic of Yalta) na kutoiruhusu Italia kuangukia mikononi mwa Moscow. Mwandishi huyu alikuwa mtu wa kwanza kutaja hadharani mtandao wa siri wa kijasusi na kijeshi wa NATO - "Gladio" na kuuhusisha na kadhia hii ya Moro. Pia alikuwa katika mlolongo wa kuandaa nyaraka kuhusu jambo hili kiundani.

Pecorelli, ambaye alikuwa na mtandao mkubwa wa marafiki kutoka kundi la "P2- Masonic Lodge", na ambaye alikuwa ni mwandishi pekee aliyeweza kupata siri nyingi na nyeti za mashirika ya kijasusi na vyombo vya usalama na serikali, aliuawa na Mafia kwa risasi nne Machi 20, 1979 mjini Rome, kwa amri ya Waziri Mkuu wa kipindi hicho aliyejihusisha na Mafia, Giulio Andreotti. Pecorelli aliuawa akiwa ndani ya gari lake aina ya "Citroƫ CX". Aliuawa ili kuzima kile kilichodaiwa alijua mengi kuhusiana na sakata la Moro.

 

Nadharia ya pili ni ile inayoihusisha serikali ya Italia kuhusika na kifo cha hasa kwa matendo yake ya kutotilia uzito jambo la kuokoa maisha ya Moro. Matendo yake, kama kusitisha kufanya mazungumzo na Red Brigade kwa madai ya kuwa serikali haiwezi kulipigia magoti kundi hilo. Pia kupuuza taarifa nyeti za kule alikofichwa wakati akishikiliwa mateka. Taarifa ya Romano Prodi, Profesa wa chuo kikuu cha, ambaye Aprili 2, 1978 wakati Moro yupo matekani, alikutana na wakufunzi wengine sita wa chuo hicho nyumbani kwa Profesa Alberto Clo karibu na mji wa Bologna. Lengo la kutano lao, lilikuwa ni kufanya uaguzi kwa kuiomba mizimu ya mababu wa chama cha DC kiwaambie kule aliko Moro.

Katika uaguzi huo, mzimu wa Prodi ulimtajia maeneo matatu fikrani mwake - Virtebo, Bolsena na Gladoli. Maeneo haya yote matatu, yapo kaskazini mwa mji wa Lazio, lakini kuna kaeneo ambako si maarufu kanaitwa Via Gladoli 96 kapo mji wa Rome - mji ambao ndio haswa iliaminika Moro anashikiliwa. Prodi hakuwahi kulifahamu jina Gladoli, lakini mzimu ulimgahamisha fikrani. Alitoa taarifa hizi za uaguzi katika makao makuu ya chama cha DC mjini Rome, idara ya masuala ya jinai ya chuo cha Bolgna, na Polisi.

Lakini jambo la kushangaza, iliwachukua polisi hadi siku nne kuchunguza eneo hilo la Via Gladoli mjini Rome, ambapo hawakubaini kitu. Lakini Aprili 18, eneo hilohilo ambalo polisi hawakukuta kitu, iligundulika jengo ambalo lilikuwa ngome ya Red Brigade, na mmoja wa viongozi wao aliishi katika jengo hilo. Hata kama Moro hakushikiliwa katika jengo hilo, lakini Prodi alikuwa sahihi kulihusisha eneo la Via Glafoli na Red Brigade. Lakini je, mizimu yake ilijuaje?

 Achilia mbali polisi kujuzwa fununu za Profesa Prodi za kwamba Moro alikuwa eneo la Via Gladoli, hilo tisa. Kumi, ni miaka miwili mbele baada ya kadhia ya Moro, ni taarifa ya mwandishi wa habari, Luca Villoresi Juni 1980 katika gazeti la "La Republica", naye alipata taarifa nyeti za ilipokuwa mahakama ya siri ya Red Brigade - alipokuwa ameshikiliwa Moro kwa siku 54. Eneo hili kusini mwa Rome, linaitwa Via Montalcini. Baada ya andiko lake, Villoresi hakuitwa ili hata kulisaidia jeshi la polisi kwa aajili ya uchunguzi. Ilikuwa kimya! Aligundua kuwa polisi walijua eneo hili tangu siku ya kwanza alipotekwa Moro, lakini hawakuchukua hatua kulivamia.

Pia, Villoresi aligundua kuwa gari iliyosemekana ni ya shirika la kijasusi la Italia, ambayo ilifungiwa vifaa vya umeme vya kiupelelezi, na ambayo hata wakati wa tukio la utekaji wa Moro ikisemekana kuwepo eneo la tukio, basi ilikuwepo eneo hilo la Via Montalcini. Villoresi alijua viongozi wa wakuu wa chama cha DC na serikali kama waziri wa mambo ya ndani, Francesco Cossiga na Waziri Mkuu, Giulio Andreotti, wanajua ukweli lakini wanafinyangafinyanga suala hili ili kuuficha ukweli wa sakata la Moro. Na hata wale waliojaribu kuibuka nakuonesha njia juu ya sakata hili, walizimwa. Huenda ni kweli walitaka Moro afe.


Akinukuliwa na gazeti la "Indipendent" la Uingerza la Octoba 22, 2011, Villoresi aliandika katika "La Rebublica": "Sakata la Moro halijaleta ufumbuzi sahihi zaidi ya kuzalisha uongo mwingi. Nafikiri ni vugumu sasa kuelewa nini kilitokea", aliandika. "Kuna watu wanaoujua ukweli, lakini hatuwezi kujua kama wanatuambia ukweli". Ni dhahiri Villoresi aliwarejelea Cossiga na Andreotti kuujua ukweli, lakini hawakutaka kuusema. Hata baada ya kufariki kwa viongozi hawa, bado kitendawili cha Moro kimebaki palepale.

Lakini jambo lingine linaihusisha serikali ya Andreotti, ni kwa wanachama wa Red Brigade waliokamatwa baadaye wakisemekana kuhusika na kadhia hii ya Moro. Walikuwa jela miaka nenda rudi, pasi na serikali kuanzisha kuwahoji ili kupelekea uchunguzi juu ya jambo hilo. Kwanini uchunguzi ulitupwa kapuni wakati pakuanzia ni hapo? Hatujui.


Pia nadharia ya kuhusika kwa serikali inakaziwa na mauaji ya Jenerali Carlo Alberto Dalla Chiesa Septemba 3, 1982. Jenerali Chiesa alifanikiwa sana kuwakamata na kusambaratisha ngome za Red Brigade kuliko yoyote. Mei 1, 1981, aliteuliwa kuwa mkuu wa jeshi wa Palermo katika kisiwa cha Sicily ili akaudhibiti mtandao wa Mafia. Unajua kwanini Chiesa alipelekwa Sicily na Waziri Mkuu Giulio Andreotti? Sicily ilikuwa ni ngome kuu ya Mafia, na katika viongozi waliotokea Italia kuwa na mahusiano na Mafia, basi ni Andreotti. Kupelekwa kwa Chiesa Sicily, alipelekwa katika mdomo wa mamba makusudi ili auawe. Na kweli, aliuawa na Mafia kwa amri ya kiongozi wao Salvatore 'Toto' Riina, miezi minne mbele tangu ateuliwe. Yasemekana Jenerali Chiesa alikuwa mmoja wa watu waliojua kiundani kuhusu sakata la utekaji na mauaji ya Moro.

Ndiyo, sakata la Aldo Moro ni mazalia ya msuguano wa vita baridi iliyoweka ombwe la kisiasa kwa Italia, nchi ambayo iliathiriwa pa kubwa na msuguano huo kuliko nchi yoyote ya Ulaya. Moro anabaki kuwa mwathirika wa msuguano huo, akiwa kama daraja la maridhiano. Akiwa na ndoto ya kuiona Italia isiyopasuka kati kiitikadi, bali yenye umoja. Akiwa na ndoto ya kutimiza kile alichokiita maridhiano ya kihistoria(historical compromise) katika nyakati za hatari. Lakini ndoto hii ilikufa siku aliyotekwa, na ilizikwa siku aliyouawa. Hata ule ushirikiano wa wa maneno tu, wa DC na PCI, ulikufa palepale. Na ukawa mwanzo wa kifo cha chama cha PCI kilichojifia taratibu sanjari na anguko la Umoja wa Kisovieti.

Katika msuguano huu wa siasa za vita baridi kwa Italia, hauwezi kuongelewa bila kutajwa kwa sakata la Moro, daraja la maridhiano lililobomolewa kabla hata ya kuvusha maridhiano yenyewe. Na kitendawili chake, cha nani hasa aliyebomoa daraja hili? Ingali masikioni mwetu tunalisikia jina la kundi la mrengo wa kushoto-mbali, la Red Brigade. Ni kundi la namna gani hili? Basi tuendelee.

Kuzaliwa na kufa kwa kundi la Red Brigade, na harakati zake.

----------------------------------------------------------------------------------------


Wakati utawala wa dikteta wa kifashisti, Benito Mussolini unahitimishwa rasmi nchini Italia mwaka 1943, baada ya miongo miwili ya figisu za bila siasa za upinzani - za kudhibiti vyama vya siasa, kufunga na kuua wapinzani wake au kuwakimbiza uhamishoni - na mika miwili mbele(1945) vita kuu ya pili ya Dunia ikifikia tamati; ilishuhudiwa mwanzo ulioleta matumaini wa ukurasa mpya wa siasa za vyama vingi na ushindani nchini humo. Siasa hizi zilianza kujengwa kwa kuandika katiba mpya mwaka 1947 iliyopitishwa na Bunge la katiba Disemba 22, na kuachapishwa katika gazeti la serikali Disemba 27. Katiba iliyovunja mamlaka ya Kifalme, na kupeleka mamlaka kwa wananchi kwa kuwa rasmi Jamuhuri, iliandikwa kwa umakini kuzuia nchi hiyo kurudi tena katika udikteta wa kifashisti au mwingine wowote. Na mwaka uliofuta(1948), ulifanyika uchaguzi mkuu ambao ulishuhudia chama cha Democrazia Cristina(DC), au Christian Democrat cha mrengo wa kati kikishinda na kushika serikali, na baadaye kiendelea kushinda kwa zaidi ya miongo minne mbele kwa msaada wa Marekani na washirika wake kwa hofu ya vita baridi.

Vyama vya mrengo wa kushoto ambavyo vilidhibitiwa barabara na serikali ya kifashisti ya dikteta Mussolini, husani chama cha kikomunisti cha Partito Comunista Italiana(PCI), au Italian Communist Party, na kile cha kisoshalisti cha Partito Socialista Italiana(PSI), au Italian Socialist Party, na vyama vinginevyo, hatimaye navyo baada ya miongo miwili vilirudi katika ulingo wa siasa vikishiriki uchaguzi huo. Uchaguzi ulioonekana kama neema ya ukurasa mpya kwa nchi hiyo, ulififia ghafla. Kwani ulikuwa mwanzo wa sakata la vita baridi iliyoingilia kati siasa hizo mpya na kuigeuza Italia  kama chumba cha mvutano wa vita hivyo kwa Ulaya - kati ya Marekani na washirika wake, dhidi ya Umoja wa Kisovieti, na kuipelekea nchi hiyo katika ombwe kuu la kisiasa kwa mapambano ya makuu ya kitabaka.