Stori

Mauaji ya Waziri Mkuu mstaafu katikati ya ombwe la kisiasa Italia: Kuzaliwa na kufa kwa kundi la RED BRIGADE (Sehemu ya Kwanza)

Ilikuwa ni Mei 9, 1978, majira ya mchana wa saa saba katika mji wa historia ya kale, wa Rome. Ambapo polisi walinasa mawasiliano muhimu ya simu kwa wakati huo, kwa Italia. Mtu asiyejulikana alipiga simu kwa mmoja kati ya wasaidizi wa Waziri Mkuu mstaafu aliyekuwa matekani, na ikiwa ni siku 54 zikiwa zimepita. Mpigaji alisema: "katika barabara ya Caetani kuna gari jekundu lina mwili wa Moro", kisha alikata simu. Kutoka makao makuu ya Polisi Rome, maafisa wake, haraka walikimbia kuelekea eneo tajwa. Walilikuta gari hilo aina ya Renault-4 likiwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara ya Michalangelo Caetani, katikati ya mji wa Rome. Eneo ambapo gari hilo lilitelekezwa, ilikuwa jirani sana na makao makuu ya vyama viwili katika mji huo - umbali wa yadi 300 kutoka makao makuu ya chama cha Waziri Mkuu aliyetekwa, cha Christian Democratic Party, au kwa kiitaliano "Democrazia Cristina (DC)", na yapata yadi 200 hadi makao makuu ya chama pinzani, na yaliyokuwa na ulinzi mkali masaa 24/7, ya chama cha Italian Communist Party, au "Partito Comunista Italiana(PCI)".

Polisi walifika eneo hilo na kuweka utepe wa rangi nyeupe na bluu kuzuia shughuli yoyote katika kiunga hicho lilipotelekezwa gari hilo, huku wakichukua tahadhari zote kulifungua. Askari wa idara ya zima moto wa jiji hilo walifungua kwa uangalifu mkubwa gari hilo na kukata mfumo wa umeme wa gari hilo kwa kukata nyaya baada ya  kipande fulani cha bodi.

Ni kwanini hasa walichukua tahadhari kulifungua gari hilo? Hofu ya mabomu ya kutegwa. Hofu ya mabomu ya kutegwa ilikuwa kuu kwa Italia kipindi hicho wakati nchi hiyo imekaa tenge kiusalama. Usalama uliodhoroteshwa na mvutano mkubwa wa kitabaka katika nyakati hizo za vita baridi - kwa mamaandamano, migomo na vurugu za mara kwa mara katika zilizozalisha makundi yenye misimamo mikali ya itikadi za kisiasa,  na yale ya siri kama P2 Masonic Lodge, sanjari na sekeseke la mtandao wa Mafia. Makundi haya, yote kwa mara mojamoja yalitumia mabomu ya kutegwa yakiwalenga wapinzani wao na watumishi wa serikali, hasa askari na majaji.

 

Basi polisi walipofanikiwa kulifungua, ni kweli, ndani yake katika buti kulilazwa mwili uliotokwa pumzi, wa Aldo Moro, waziri mkuu mstaafu wa Italia, ukiwa umevishwa suti nadhifu ya rangi ya bluu iliyokoza, shati la mikono mifupi na tai nyeusi, na kwa juu koti kubwa na refu. Ni kwamba, suti hiyo ni ile aliyovaa asubuhi ya tarehe 16 Machi ya mwaka huo - siku 54 nyuma aliyotekwa akiwa njiani kwenda Bungeni.


Ndani ya gari hilo, mwili wake ukilazwa Katika buti, kichwa chake kilifunikwa kwa blanketi. Na pembeni yake kulikuwa na mfuko wa plastiki ukiwa na vifaa vyake vidogo - saa, wembe, na vinginevyo. Alilala juu ya dimbwi la damu zilizoanza kukauka, lakini zikinuka ubichi. Damu zilizotoka katika matundu kumi ya risasi kifuani mwake. Kwa taarifa ya polisi, ilionesha aliuawa kwa kupigwa risasi jana yake. Taarifa za polisi zinaonesha alipigwa risasi kabla ya kuvalishwa koti hilo refu na kupakiwa garini, kwa kuwa koti hilo halikutobolewa na hata tundu moja la risasi. Zaidi, ilihisiwa huenda alipigwa risasi mazingira ya fukwe katika mji huo na kisha mwili wake kuburuzwa kabla ya kupakiwa garini, kwa kuwa katika pindo za miguu ya suruali yake kulikutwa mchanga mwingi wa fukwe.