Habari

Mapinduzi Myanmar: Waandamanaji 38 Wauwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama

Waandamanaji wamekuwa wakishinikiza kukomeshwa kwa utawala wa kijeshi na kuachiliwa huru kwa viongozi wa nchi hiyo waliochaguliwa akiwemo Aung San Suu Kyi ambaye aling'olewa madarakani na kuzuiliwa wakati wa mapinduzi

Jumla ya vifo 38 vimeripotiwa baada ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama kuwafyatulia risasi Waaandamaji wanaopinga Utawala wa Kijeshi katika Miji kadhaa nchini Myanmar.

Waandamanaji wamekuwa wakishinikiza kukomeshwa kwa utawala wa kijeshi na kuachiliwa huru kwa viongozi wa nchi hiyo waliochaguliwa akiwemo Aung San Suu Kyi ambaye aling'olewa madarakani na kuzuiliwa wakati wa mapinduzi.

 “Leo ni siku ya umwagikaji damu mkubwa kushuhudiwa tangu mapinduzi yatokee Februri 1. Leo, ndani ya siku moja tu- watu 38 wamefariki. Tuna watu Zaidi ya 50 ambao wamefariki tangu mapinduzi yatokee” huku wengi wakiwa wamejeruhiwa, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar Christine Schraner Burgener, alinukuliwa na waandishi wa habari siku ya jumatano.

Mapinduzi hayo na kutumia kwa nguvu dhidi ya waandamanaji yamekuwa yakilaaniwa kimataifa lakini majeshi ya Myanmar yamekuwa yakiendelea kupuuza.