Afrika

Maoni: Kenya Inavyokuja Juu kwenye Muziki Afrika Mashariki, Wasanii wa Tanzania Wanapaswa Kujifunza

Kuna mengi ya kuboresha lakini tuanze na ubunifu kwani ubunifu ukidumaa itatufanya kutumia nguvu kubwa sana kukuza sanaa yetu na kuingia katika ushindani

Muziki ni sanaa, muziki ni utamaduni, muziki ni maisha, muziki ni ajira, muziki ni rafiki wa kweli kwenye shida na raha. Kuna mambo mengi yanayoweza kuamsha homoni za hisia mbalimbali, hisia tamu na chungu kwa nyakati tofauti. Muziki umedhihirika kuwa na nguvu katika jamii nyingi hasa kwenye kuelimisha, kuburudisha, kufariji, kuhamasisha na kuchechemua mabadiliko katika jamii husika.

 

Muziki umekuwa kielelezo cha jamii na utamaduni wao. Barani Afrika na katika mabara mengine muziki umetumika kikamilifu kuwasilisha tamaduni kwa jamii nyingine. Duniani kote muziki umepevuka kutoka kuwa sanaa pekee na kuwa biashara. Wasanii na wadau wengine katika sekta ya sanaa wanaweza kuvuna kutoka katika sekta ya muziki kupitia kazi zao. Hata hivyo mbali na muziki kuwa biashara bado haiondoi ladha yake ya kuwa kiwakilishi cha jamii ama utamaduni fulani.

 

Kuna mifano kadhaa, duniani pote ukisika muziki wa mahadhi ya raggae tayari watu wanahusisha na utamaduni wa Jamaica, ukisikika muziki wa HipHop watu wanahusisha na utamaduni wa watu weusi wa Marekani, ukisikika muziki wa country unahusishwa zaidi na waingereza, muziki wa salsa…. Barani Afrika muziki wa zuku na rhumba unahusishwa zaidi na mataifa ya Congo wakati muziki wa kwaito unahusishwa moja kwa moja na tamaduni za jamii ya kusini mwa Afrika.

 

Inaweza kuwa suala lisilofurahisha kwenye masikio ya wengi hasa tukiuzungumzia muziki kama kiwakilishi cha tamaduni Fulani kwani muziki pia umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuvuka na kugalagaza tamaduni zingine. Mfano mahadhi ya raggae hayaimbwi Jamaica pekee bali duniani kote. Mahadhi ya Hip Hop na mahadhi mengine yametapakaa duniani kote.

 

Basi tukubaliane tuu kutokukubaliana kwamba mahadhi ya muziki yameponyoka kutoka tamaduni moja na sasa yanaweza kutumika na tamaduni zaidi ya moja. Ingawa tunapaswa kuwa makini hapa; haimaanishi kwamba mahadhi haya hayana asili, bado asili ya mahadhi haya yatabaki vizazi na vizazi.

 

Katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki muziki wetu umekumbwa na mchanganyiko wa mahadhi, kuna kila aina ya mahadhi na hii inaweza kuwa kwa sababu za kihistoria na utandawazi. Muziki wetu umeathiriwa na mahadhi mengi sana, hata hivyo haimaanishi kwamba hatuna muziki wa asili katika ukanda huu. Mahadhi kama taarab, zuku rhumba na mengine ni miongoni mwa mahadhi yanayowakilisha zaidi ukanda huu.

 

Kwa sasa mambo yamebadilika kutokana na utandawazi na tunakubali kwamba mahadhi si jambo la kuzingatia sana ingawa ni hamu ya kila jamii kupenyeza na kukuza utamaduni wake nje ya mipaka yake kama ilivyo kwa Tanzania na hamu ya kukuza zaidi lugha ya Kiswahili. Kwa sasa tuna Afro-Pop ambayo ni mahadhi ya muziki wa Kiafrika, wasanii katika ukanda wetu pia wana uhuru wa kuimba mahadhi mbalimbali.

 

Kufanana kwa mahadhi ya muziki wa mataifa haya ya Afrika Mashariki haimaanishi kwamba hakuna ushindani baina ya mataifa haya. Tanzania, Kenya na Uganda zimekuwa katika nafasi nzuri kimuziki miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki. Kuanzia miaka ya 1990 ambapo muziki wa kizazi kipya ulianza kushika kasi wanamuziki wa Tanzania kama wakina Lady Jay Dee, TID, AY, Professor Jay, Dully Sykes na sasa wakina Diamond, Alikiba, Harmonize, Nandy na Zuchu wameonekana kuipeperusha vyema bendera ya Afrika Mashariki.

 

Kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imebarikiwa kumpata mwanamuziki ambaye ameiwakilisha vyema barani Afrika na sehemu kubwa ya dunia. Si mwingine ni Diamond Platnumz, Diamond amekuwa darasa kwa wasaniii wengi wa Afrika Mashariki na hata Afrika kwa ujumla hasa katika kutengeneza muziki uliovuka mipaka. Mbali na muziki Diamond amekuwa kioo katika kufanya biashara ya muziki hasa kupitia mitandao kama YouTube na mingine.

 

Kwa upande wa majirani wa Tanzania hasa Kenya wamekuwa na maendeleo mazuri ya ukuaji wa muziki wao. Kundi la Sauti Sol wamekuwa wakipeperusha vyema bendera ya muziki wa Kenya. Ukuaji wa muziki kati ya Tanzania na Kenya unatofautiana kwa namna kuu mbili; wanamuziki wa Tanzania wanajitutumua kulifikia soko la dunia kwa namna ambazo zinawaletea matokeo ya muda mfupi wakati Kenya bila shaka wamewekeza katika matokeo ya muda mrefu.

 

Tukianza na kuangazia muziki wa Kenya, wasanii wa Kenya wameubeba u-Kenya kupitia muziki wao; hawaimbi mahadhi ya tofauti lakini kuna ufundi mkubwa katika utunzi wa kibunifu na hata katika namna ya uwasilishaji wa kazi zao. Wanamuziki wa Kenya wanaonekana kutambua jambo wanalolitaka kupitia kazi yao ya muziki na pia wanatazama uendelevu zaidi kuliko matokeo ya haraka ambayo hayana mwendelezo mzuri.

 

Wanamuziki wa Tanzania wamewazidi wenzao wa Kenya kwa takwimu lakini katika ubora wa sanaa Kenya wametengeneza daraja lao ambalo mashabiki watakaposhituka wasanii hao watavuna pesa nyingi kutoka katika majukwaa ya muziki. Kuna jambo zuri ambalo litaufanya muziki wa Tanzania kuendelea kukua, jambo hili ni kuanzishwa kwa lebo zinazosimamia na kukuza wasanii.

 

Kupitia lebo kama WCB, Konde Gang na nyingine kuna uwezekano wa kutumia ushindani uliopo kukuza vipaji vingi zaidi. Kinacholeta ukakasi katika hili ni mikakati ya namna ya kukuza vipaji hivyo, je lebo hizi zinatumia njia za kimkakati za sanaa kukuza vipaji au lebo zote zinategemea kiki?

 

Tusizungumzie kiki, ni jambo lenye mjadala mpana. Tutazame lebo ya Sol Generation na jinsi ambavyo inaibua vipawa vyenye uwezo mkubwa wa uandishi na uimbaji unaoshitua masikio mengi. Vipawa vya wasanii kama Ben Sol na Nviiri the Story Teller ni wachache ambao kazi zao chache zimekuwa gumzo kwa wachambuzi wa muziki.

 

Tukiachana na Sauti Sol kuna wanamuziki kama kina Otile Brown ambao wananyanyasa sana wapenzi wa muziki wa taratibu kwa vibao vikali vya mara kwa mara. Kwa kutazama mbali muziki wa Kenya unaweza kuwa ndio muziki unaopendwa zaidi kutokana na ubunifu katika uandishi na hata uwasilishaji.

 

Wakati Tanzania ikiwa na faida ya kuwa na wasanii wengi zaidi wenye majina na uwezo mkubwa wa sanaa bado kuna ombwe kubwa la ubunifu kuanzia kwenye uandishi tunaweza kusema kuna kigugumizi cha uandishi. Wandaaji wa midundo na video wanafanya kazi kazi kubwa lakini maudhui yetu yamekuwa kama moshi kufuka kwa muda na kisha kupotea kabisa.

 

Wasanii wa Tanzania wanapaswa kuboresha uandishi wa kazi zao, wachache kama Mbosso na Barnaba wana uandishi mzuri lakini wanapaswa kuongoze ubunifu kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa juu katika sekta zote kimuziki.

 

Kuna mengi ya kuboresha lakini tuanze na ubunifu kwani ubunifu ukidumaa itatufanya kutumia nguvu kubwa sana kukuza sanaa yetu na kuingia katika ushindani. Wakati tukitafakari tuchukue muda kusikiliza muziki wa Kenya na Tanzania halafu turudi hapa tukiwa na maoni kuhusu muelekeo wa muziki wetu.