Habari

Mama Samia Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Samia Suluhu Hassan ambaye alivunja historia kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke mwaka 2015 amevunja rekodi kubwa zaidi kwa kuwa Rais wa Tanzania.

Machi 19, 2021 ni tarehe ambayo taifa la Tanzania limeandika historia mpya baada ya kupata Rais wa kwanza mwanamke. Tangu uhuru na muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawahi kutokea kuwa na Rais mwanamke.

 

Samia Suluhu Hassan ambaye alivunja historia kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke mwaka 2015 amevunja rekodi kubwa zaidi kwa kuwa Rais wa Tanzania. Samia Suluhu Hassan ambaye hujulikana zaidi kama Mama Samia, ameapishwa rasmi Machi 19,2021 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

 

Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride mara baada ya kuapishwa. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makamu wa Rais ndiye anapaswa kuchukua nafasi ya Rais endapo Rais atashindwa kwa sababu yoyote kuendelea kuongoza nchi. Wakati wa kuapishwa kwake Mama Samia amewataka Watanzania kuungana katika kujenga nchi.

 

Samial Suluhu Hassan aliingia rasmi katika ulingo wa siasa mwaka 2000 wakati alipochaguliwa kwenye baraza la wawakilishi la Zanzibar kama mjumbe maalum. Nyota yake ilianza kung’ara katika medani za kisiasa na uongozi ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuteuliwa kuwa waziri wa Afya, Jinsia na Watoto. Uteuzi uliofanywa na Rais wa kipindi hicho ulimfanya kuwa mwanamke pekee kaliyeshika nyanjifa ya juu.  

 

Mwaka 2005 alichaguliwa tena kuwa mjumbe maalum na kuteuliwa kuwa  waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mwaka wa 2010 aliwania na kushinda nafasi ya Ubunge na kuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

 

2010 aliteuliwa katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa maswala ya muungano katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihudumu chini ya Makamu wa Rais Mohamed Gharib Bilal.

 

2014 wakati Tanzania ikiwa kwenye mchakato wa Mabadiliko ya Katiba Samia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.