Habari

Majaliwa: Tukiongeza Mishahara Gharama za Maisha Zitapanda

Waziri Mkuu asema serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi katika maeneo mengine ambayo ni zaidi ya mishahara

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi tofauti na kuongeza mishahara. 

Akijibu swali la Mbunge wa Konde kupitia chama cha ACT Wazalendo, Khatibu Said Haji aliyetaka kujujua ni lini serikali itaongeza mishahara kwa wafanyakazi nchini katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni Dodoma, Waziri Mkuu amesema kuwa kuna njia nyingi za kuboresha maslahi ya wafanyakazi ikiwemo kuwapandishamadaraja na kuwapunguzia kiwango cha kodi. 

Majaliwa ameongeza kuwa hakuna haja ya kutangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi hadharani kwani kunaongeza gharama za maisha na kusababisha vitu vingi kupanda bei bila sababu ya msingi.

"Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi katika maeneo mengine ambayo ni zaidi ya mishahara, na niwaombe wafanyakazi nchini wasikate tamaa kwa kusubiri watangaziwe hadharani," amesema Majaliwa.