
Afisa Maendeleo ya Jamii
Wilaya ya Kigamboni, Happy luteganya amewataka Maafisa maendeleo, watendaji na
maafisa ustawi wa kata kuwa chachu ya utatuzi wa matatizo ya Afya ya uzazi
yanayowakabili walemavu katika maeneo yao
Akizungumza katika uzinduzi
wa Mradi wa Uchechemuzi wa Haki ya afya salama ya uzazi kwa watu wenye ulemavu
katika manispaa ya Kigamboni utakaotekelezwa katika kata zote za
manispaa hiyo uliobuniwa na Taasisi ya Building Inclusive Society Tanzania
Organization (BITSO) Afisa huyo amesema kuwa watendaji hao wanapaswa
kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa maafisa wa BITSO
watakaofika katika utekelezaji wa Mradi huo.
"Tutapitishwa kwenye
Mradi naomba tuupokee tukausimamie kulingana na malengo ambayo yamepangwa"
amesema Luteganya.
katika hatua nyingine,
Luteganya amewashukuru BITSO kwa uzinduzi wa Mradi huo katika wilaya ya
Kigamboni kwani wangeweza kuutekeleza mradi huo katika wilaya nyingine lakini
wameamua kuanza na wilaya ya kigamboni hivyo wilaya hiyo inapaswa kuwa ya mfano
ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo katika maeneo mengine.
Mratibu wa Mradi huo, Rajabu
Mpilipili amesema kuwa mradi huo utahusisha mafunzo mbalimbali kwa watu
wenye ulemavu na wasio na ulemavu kwani watu wasio na ulemavu ndio
wanaoishi na watu wenye ulemavu katika Jamii hivyo nao pia ni wadau Muhimu
katika suala hilo
Mpilipili, amesema kuwa
kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa afya salama ya uzazi kwa watu wenye
ulemavu na wengi hawapewi haki zao za msingi zinazohitajika hivyo taasisi hiyo imekuja
na Mradi huo ili kuwawezesha walemavu kupata haki hizo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya BITSO, Pascal Majula Silvester amesema kuwa Taasisi hiyo inamalengo ya kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata huduma ya Afya kwa usalama zaidi kama haki yao ya msingi ya kibinaadamu na kueleza kwamba Taasisi hiyo imejikita zaidi katika kuwasaidia walemavu kupata haki zao za msingi.
Leave a comment