Habari

Lipumba amkumbusha Rais Magufuli kumaliza kiporo cha Katiba ya Wananchi

Awataja Kabudi, Samia Suluhu, Polepole na Tulia kuwa viungo muhimu katika kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba ametoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kukamilisha mchakato wa Katiba ya Wananchi. Akizungumza jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Jumatatu Februari 1, 2020, Prof. Lipumba amemweleza Rais Magufuli kwamba mambo makubwa aliyoyafanya na anayoendelea kuyafanya katika kipindi chake cha uongozi yataendelezwa na kulindwa endapo kutakuwa na ‘Katiba ya Wananchi’. 

 

“Nakuombea kwa moyo wa dhati kabisa, Mungu akupe nguvu katika kipindi hiki ili uweze kutekeleza viporo vyote ulivyovibakisha. Unapomaliza kipindi chako watu watakaoweza kuyalinda mafanikio uliyoleta katika nchi yetu, watatokana na Katiba iliyotokana na mapendezo ya wananchi wa Tanzania,” amesema Prof. Lipumba.

 

Prof. Lipumba amesisitiza kwamba anaamini suala la kukamilisha mchakato na kupatikana kwa Katiba ya Wananchi ni rahisi hasa kwa kuzingatia kwamba Rais Magufuli mwenyewe alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Mabadiliko ya Katiba wakati Makamu wa Rais Samia Suluhu alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Mabadiliko ya Katiba. 

 

“Natoa wito, na kwa bahati wewe mwenyewe ulikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Na Mama Samia [Makamu wa Rais] ndiye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Kuna wazee wazito kina Prof. Kabudi…ndio walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba. Kuna vijana wako, Polepole. Naibu Spika tena tulikuwa naye kwenye kamati moja. [Hawa wote wanaweza kukusaidia katika kuhakikisha mchakato wa Katiba ya Wananchi unakamilika],” ameeleza Prof. Lipumba.

 

Akimalizia hotuba yake fupi, Prof. Lipumba amesisitiza kwamba ana uhakikia hekima itamwongoza Rais Magufuli ili kutekeleza matakwa ya wananchi ya Katiba Mpya na kuiachia nchi urithi wa Katiba Mpya atakapomaliza muda wake.

 

“Nina uhakika, kwa kuwa jambo hili ni la kwako sio la kwangu-lipo katika hotuba zako. Nina uhakikia jambo hili utalishughulikia na utatuachia urithi wa Katiba inayotokana na maoni ya wananchi. Nakushukuru na nakuombea kwa mwenyezi Mungu akupe afya, akupe hekima, akupe Subira ili uweze kukamilisha mambo yote haya ambayo wanayapenda Watanzania,” amesisitiza Prof. Lipumba. 

 

Mchakato wa upatikanaji wa Katiba ya Wananchi ulianzishwa rasmi na Serikali ya awamu ya nne mwaka 2011 kufuatia maoni ya wananchi kwamba Katiba iliyopo ina mapungufu mengi. Hata hivyo, mchakato huo ambao uliibua mvutano mkubwa wa hoja miongoni mwa wananchi haukukamilika na sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mchakato huo kuingiliana na uchaguzi mkuu wa 2015. Vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM) viliahidi kuendeleza mchakato huo endapo vingeshinda na kukabidhiwa madaraka. 

 

Baada ya uchaguzi kumalizika mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa kwani CCM ambao walishinda walisema kwamba Katiba Mpya haikuwa kipaumbele.