Michezo

Ligi kuu Uingereza: Mashabiki Kurejea Viwanjani Kabla ya Msimu Kumalizika.

Mkurugenzi mkuu wa ligi kuu Uingereza, Richard Masters anaamini mashabiki wanaweza kurejea viwanjani kushabikia timu zao kabla ya msimu huu wa 2020/21 kuisha.

Mechi zote za ligi nchini humo zinachezwa bila mashabiki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.

Utaratibu wa kuruhusu mashabiki angalau elfu mbili viwanjani uliwekwa baada ya serekali ya Uingereza kuigawa miji kutokana na ngazi na hali ya mlipuko wa COVID-19. Utaratibu huu ulisitishwa ghafla baada ya visa vingi kuripotiwa nchini humo hali iliyopelekea nchi hiyo kuweka tena marufuku ya kutoka nje.

Katika mahojiano yake na gazeti la Financial Times Bwana Masters alisema "Nina imani mashabiki watarejea viwanjani"

"Hakuna mtu anayeweza kutabiri kwasababu hili janga (COVID-19) lina namna nyingi za kukushangaza, ila sisi hatujapoteza matumaini na tunaweza kuona mashabiki kadhaa viwanjani msimu huu"- Richard Masters

"Natumaini msimu ujao utaanza haraka na tutaona pia mashabiki katika idadi kamili kama zamani na hapo tutakua tumerejea katika uhalisia wa ligi kuu Uingereza ( Premier League)" Masters aliongeza.(Richard Masters:Mkurugenzi mkuu wa ligi kuu Uingereza)

Kwa sasa mechi zote za ligi kuu zinaonyeshwa kupitia vituo mbalimbali vya television ikiwa ni mpango unaofahamika kama 'Project Restart' tangu ligi hiyo iliporejea tena June 2020 na utaratibu huu utadumu hadi mashabiki watakapo rejea viwanjani. 

Mashabiki wamekosekana viwanjani kwa kiasi kikubwa tangu ligi hiyo iliporejea mwezi June 2020.

Mwezi Oktoba 2020 baadhi ya mechi zilishuhudiwa na mashabiki wasiopungua elfu mbili lakini baadae utaratibu huo ulifutiliwa mbali baada ya nchi hiyo kuweka marufuku kutoka nje kwa mara ya pili.

Kwa sasa Uingereza ipo katika marufuku ya tatu ya kutoka nje kutokana na COVID-19, Waziri Mkuu Boris Johnson atatoa kanuni mpya za kukabiliana na janga hilo siku ya Jumatatu tarehe 22 mwezi huu.