Duniani

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ashindwa kushiriki mazishi ya mama yake mzazi kwa sababu ya corona

Klopp ameshindwa kushiriki maziko ya mama yake kwa sababu Ujerumani wamezuia wasafiri wote kutoka Uingereza kuingia Ujerumani kutokana na mlipuko wa aina mpya ya kirusi cha corona nchini Uingereza

Jurgen Klopp amempoteza mama yake mzazi Elisabeth Klopp ambaye amefariki akiwa na miaka 81 na kuzikwa siku ya Jumanne Februari 9 nchini Ujerumani. Klopp ameshindwa kushiriki maziko ya mama yake kwa sababu Ujerumani wamezuia wasafiri wote kutoka Uingereza kuingia Ujerumani kutokana na mlipuko wa aina mpya ya kirusi cha corona nchini Uingereza. 

 

Meneja huyo wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza ameomboleza kifo cha mama yake kwa kusema kwamba mama yake alikuwa mtu wa pekee sana katika maisha yake. Hata hivyo, Klopp ameviambia vyombo vya habari vya Ujerumani kwamba hali ya mlipuko wa Covid-19 itakapotengemaa atafanya sherehe ya kuenzi maisha ya mama yake. 

 

Awali mwezi huu Klabu ya Liverpool ilinyimwa ruhusa ya kuingia Ujerumani kucheza mchezo wake wa mwisho wa hatua ya 16 bora katika michuano ya klabu bingwa Ulaya (UEFA) kutokana na zuio la wasafiri kutoka nchi zenye aina mpya ya virusi vya corona. Mchezo wa Liverpool na RB Leipzig hautachezwa Ujerumani na badala yake utachezwa Februari 16 katika uwanja wa Puskas jijini Budapest nchini Hungary.