Habari

Kenya Yapokea Shehena ya Kwanza ya Chanjo ya Corona

Chanjo hiyo ilisafirishwa na UNICEF kupitia mpango unaolenga kusambaza chanjo Ulimwenguni kote unaojulikana kama COVAX.

Akizungumza kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumanne usiku wa manane wakati shehena milioni 1.02 ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca ilipowasili, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alisema Kenya ni kama ilikuwa ikipigana vita na Covid na risasi za mpira, lakini kwa chanjo hiyo, sasa ni sawa na risasi halisi.

Waziri Kagwe aliongozana na Waziri wa Usafiri, James Macharia na mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, Rudi Eggers. Kagwe aliishukuru UNICEF ​​na WHO kwa kufanya kazi na Kenya kufanikisha ufikiaji wa chanjo ya Oxford-Astrazeneca.

Ndege ya Qatar Airways QR1341 ilitua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta majira ya saa 5 usiku ikiwa imebeba chanjo ya  Oxford-Astrazeneca ambayo inaonekana kuwa na ufanisi zaidi zaidi maeneno ya Afrika na katika nchi hiyo kipaumbele kitatolewa kwanza kwa wafanyakazi wa afya wakifutiwa na wafanyakazi  wengine walio mstari wa mbee katika kufanya shughuli za jamii; polisi na walimu.

Katika bara la Afrika shehena ya Chanjo imezifikia mataifa ya Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Angola kupitia mpango wa kimataifa wa usambazaji chanjo, Covax.

Kupitia mpango huo, Nigeria imepokea dozi milioni nne, Jamhuri ya Kidemokrasia imepokea dozi milioni 1.7, Angola imepokea zaidi ya dozi 600,000 wakati Gambia ikitarajia kupokea kiasi dozi 30,000.

Wiki iliyopita, Ghana na Ivory Coast zilikuwa nchi za kwanza barani Afrika kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kupitia mpango huo wa Covax, ambao unalenga kusamba dozi bilioni mbili kufikia mwishoni mwa mwaka huu.