
Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri
Charles Kitima amesema kuwa ndani ya miezi miwili iliyopita zaidi ya mapadri
25, masista na manesi 60 na wenyeviti wawili wa Baraza la Walei wamefariki
dunia kwa sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya upumuaji.
Katibu wa TEC ameyasema hayo leo hii kupitia mkutano na
wanahabari na amesisitiza kuwa tishio la corona bado lipo Tanzania na Kanisa na
ongezeko la vifo bado linaendelea kuripotiwa ikiwemo ndani ya Kanisa lenyewe
''Ndani ya miezi iliyopita Mapadri 25 wamepoteza maisha
kwa matatizo ya kupumua. Masisita na manesi zaidi ya 60. Vifo vinaendelea, tuchukue
tahadhari." Alinukuliwa
Kanisa hilo limeonya kuwa, kuendelea kufanya mzaha katika
janga kama hilo ni hatari na kusisitiza kuwa elimu ya kutosha inapaswa
kuendelea kutolewa kwa kila mwananchi.
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu Kanisa Katoliki nchini
Tanzania kutoa tamko juu ya ugonjwa wa virusi vya corona nchini humo. Tamko la
kwanza lilitolewa kwa njia ya waraka mwezi Januari ambapo Raisi wa TEC Askofu
Gervaas Nyaisonga alitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona.
Katika waraka huo kanisa lilisitiza Tanzania si kisiwa na kutaka tahadhari zote
za kisayansi kuchukuliwa.
Onyo hilo la kanisa la katoliki linakuja huku Shirika la
Afya Duniani "WHO" likiendelea kutoa wito kuitaka Tanzania kuchukua
hatua zaidi kukabiliana na Covid-19.
Leave a comment