Habari

Joe Biden Afanya Mazungumzo ya Simu na Rais Kenyatta

Biden amemwahidi Kenyatta kuwa taifa lake lipo tayari kuendelea kushirikiana na Kenya kuhakikisha uthabiti wa ukanda

Rais wa Marekani amefanya mazungumzo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta siku ya Ijumaa na kumhakikishia ushirikiano thabiti wa Marekani na Kenya.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ikulu ya White House, Biden amesisitiza kuendelea kuiunga mkono Kenya katika kusimamia amani ya ukanda huo, ikiwamo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Biden ameupongeza uongozi mzuri wa Kenya katika eneo la Pembe ya Afrika pamoja na juhudi za taifa hilo kupambana na ugaidi, kukuza uchumi, kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kusimamia maendeleo endelevu.

Rais Biden na Kenyatta pia wamezungumzia hali ya kuporomoka kwa haki za kibinadamu katika eneo lenye mgogoro la Tigray nchini Ethiopia na umuhimu wa kuepuka kupotea zaidi kwa maisha katika eneo hilo na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kiutu. Vilevile, viongozi hao wamezungumzia ushirikiano zaidi katika masuala ya uthabiti wa kiukanda.