Habari

Japan Yawaenzi Wahanga wa Tsunami wa Mwaka 2011

Watu waliokuwa wamebeba maua walionekana siku ya alhamis wakitembea kwenda pwani na makaburini kuwaombea ndugu na jamaa zao waliofariki ndani ya majanga matatu yaliyoikumba nchi hiyo

Japan leo imeadhimisha miaka 10 tangu kutokea kwa janga baya zaidi la asili katika historia ya nchi hiyo ambalo ni  tetemeko kubwa la ardhi, tsunami na kuyeyuka kwa nyuklia lililoathiri taifa hilo.

Siku ya leo Japan imeadhimisha miaka 10 tangu kutokea kutokea kwa majanga matatu makubwa kuwahi kurekodiwa nchini humo. Maadhimisho hayo yamelenga kuwakumbuka wahanga takribani 20,000 wa tetemeko kubwa la ardhi, tsunami na kuyeyuka kwa nyuklia lililoathiri taifa hilo mnamo machi 11, 2011.

Watu waliokuwa wamebeba maua walionekana siku ya alhamis wakitembea kwenda pwani na makaburini kuwaombea ndugu na jamaa zao waliofariki ndani ya majanga matatu yaliyoikumba nchi hiyo.

Maadhimisho hayo ya muongo mmoja wa janga hilo baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo yamefanyika kupitia hafla za umma  huku kimya  kikitawala kwa takribani dakika 1 mwendo wa saa 14.46 nchini humo hii ikiwa ni saa kamili lilipotokea tetemeko kubwa la ardhi la ukumbwa wa 9.0 katika kipimo cha ritcher.

Mjini Tokyo, hafla ndogo itakayozingatia sheria za kuthibiti kuenea kwa virusi vya corona itaandaliwa katika ukumbi wa michezo wa kitaifa huku hotuba zikitolewa na mfalme Naruhito na waziri mkuu Yoshihide Suga huku idadi ya wageni waalikwa ikiwa ndogo kuliko kawaida.

Takribani watu 20,000 waliuawa na wengine kutojulikana walipo katika janga hilo huku wengi wakisombwa na mawimbi makali yaliofunika maeneo ya Pwani ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo. Tetemeko hilo lilisababisha tsunami kubwa ambayo ilifika hadi sehemu ya nchi kavu na kusababisha kuyeyuka kwa nyuklia katika kiwanda nyuklia cha Fukushima Daiichi na kulazimisha zaidi ya wakazi 160,000 kukimbia makazi yao pindi mionzi ilipoanza kusambaa hewani.