Habari

Ethiopia: Wanahabari Wanne Wakamatwa Kufuatia Mzozo wa Tigray

Mamia wameuawa na makumi ya maelfu kuwachwa bila makao katika vita hivyo, na kuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuripotiwa kwa ukatili na kuenea kwa mzozo mbaya wa kibinadamu

Tigray imekuwa uwanja wa mapigano tangu mnamo November 2020 pindi Waziri Mkuu, Abiy Ahmed alipotangaza hatua za kijeshi dhidi ya TPLF na akiwashtumu kuvamia jeshi la serikali kuu ya Ethiopia.

Mgogoro huo uliongezeka baada ya wapiganaji wa TPLF kudhibiti kambi moja ya wanajeshi wa serikali katika jimbo la Tigray.

Mamia wameuawa na makumi ya maelfu kuwachwa bila makao katika vita hivyo, na kuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuripotiwa kwa ukatili na kuenea kwa mzozo mbaya wa kibinadamu.

Aidha, Ethiopia iliweka vikwazo dhidi ya vyombo vya habari kwa kuzima huduma ya mtandao na kuzuia uhuru wa kutoa taarifa.

Baada ya kuzuiwa kwa vyombo vya habari vya kimataifa kwa mwezi mmoja kuingia katika jimbo hilo, serikali wiki iliopita iliwaruhusu wanahabari wa kimataifa kuripoti kutoka Tigray.

Hata hivyo, vyombo hivyo vilipewa onyo la mapema kuwa wafanyakazi wake wanaweza wakakumbwa na adhabu endapo hawatozingatia vigezo vilivyobainishwa na nchi husika.

Waliokamatwa ni watafsiri waliokuwa wakifanya kazi na waandishi wa habari wa AFP na Financial Times siku ya Jumamosi, Fitsum Berhane na Alula Akalu, Mtu wa tatu alikuwa mwandishi wa habari anayeitwa Temrat Yemane ambaye alikamatwa Mekele, mji mkuu wa Tigrayan na mwishoni mwa jumatatu Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilitangaza kuwa mwandishi wake wa habari naye ameshikiliwa nchini humo.

Baadhi ya wafanyakazi hao wanashikiliwa katika chuo cha kijeshi karibu na mji wa Makele.

Kiongozi wa Serikali ya Mpito katika eneo hilo hakuweka wazi ni kwa nini wamekamatwa lakini amesema kuwa wapo chini ya uchunguzi na kuwa kuna ushahidi ambao umeshapatikana bila kuweka wazi ni ushahidi gani.

Chombo cha habari cha Financial Times kilisema katika taarifa fupi kwamba kilikuwa ''kinachukua kila hatua'' ili kuhakikisha kwamba wakalimani hao wanaachiwa.

Licha ya waziri mkuu Abiy kutangaza ushindi baada ya wanajeshi wa serikali kuukomboa mji mkuu wa jimbo hilo Mekelle mwezi Novemba, ghasia zimekuwa zikiendelea katika eneo hilo huku hali ya hatari ikiwa bado imesalia.