Habari

DRC Congo: 60 Mbaroni Wakishinikiza Umoja Wa Mataifa Kuondoa Vikosi Vyake

Mamia ya Vijana wamekuwa wakiandamana kwa siku kadhaa katika Miji tofauti ikiwa ni pamoja na Beni, Kivu Kaskazini na Goma katika Nchi hiyo wakiwa wamekasirishwa na Kitendo cha kikosi cha Umoja wa Mataifa kushindwa kuzuia mashambulio na kuvimaliza vikundi hivyo vya waasi kwa zaidi ya muongo mmoja sasa

Polisi katika Mji wa Beni Mashariki mwa Kongo wamewakamata Watu 60 na kuwatawanya waandamanaji wanaoshinikiza kuondoka kwa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO) kwa sababu ya kushindwa kuzuia mashambulio ya waasi kwa raia wa Jamhuri ya Kongo.

Mamia ya Vijana wamekuwa wakiandamana kwa siku kadhaa katika Miji tofauti ikiwa ni pamoja na Beni, Kivu Kaskazini na Goma katika Nchi hiyo.

Waandamanaji wamekasirishwa na Kitendo cha kikosi cha Umoja wa Mataifa kushindwa kuzuia mashambulio na kuvimaliza vikundi hivyo vya waasi kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Clovis Mutsova, mmoja kati ya Waandamanaji wa kikundi cha Wanaharakati kinachojulikana kama Lucha alisema "Tunataka vitu Viwili tu, MONUSCO aondoke na Serikali ya Kongo ichukue Jukumu lake ili tuweze kuwa na Amani."

Pia, Mwanzoni mwa Mwezi huu mwanaharakati mmoja wa asasi za kiraia katika Maandamano ya Beni alisema "Tunalaani kutofaulu kwa Kikosi cha MONUSCO, Kikosi ambacho kina Uwezo mkubwa lakini kwa miaka mingi kimeshindwa kufanya chochote, hii inakera. MONUSCO lazima achukue hatua au afungashe Virago.” Depaul Bakulu

Aidha, Meya wa Beni, Modeste Buhindo Bakwanamaha pia aliliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba "Vijana wamefunga karibu Barabara zote kutaka Umoja wa Mataifa kuondoka Eneo hili, kwani bado linakumbwa na Mauaji."

Habari kutoka Kivu Security Tracker zinadai kuwa zaidi ya Watu 330 wameuawa hadi sasa kwa Mwaka huu tu katika Vurugu hizo.

Msemaji wa Polisi wa Eneo hilo, Nasson Murara alisema Maafisa walikuwa wameondoa vizuizi na kukamata takribani watu.

Mtafiti Mwandamizi wa haki za binadamu nchini Kongo, Thomas Fessy amelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja wale wote waliokamatwa, kupitia Mtandao wake wa Twitter ameandika "Ukandamizaji mkali wa maandamano ya amani leo huko Beni, Goma na Butembo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu."

Aliongeza kwa kusema "Watu wa Mashariki mwa Kongo wamechoka na Ghasia na Mauaji yasiyokoma, haswa katika Eneo la Beni. Ni Haki yao kuandamana kwa Amani kudai kwamba Serikali na walinda Amani wa Umoja wa Mataifa walinde zaidi Raia.”

Mnamo Desemba 2019, Watu kadhaa waliuawa huko Beni na Goma wakati waandamanaji wenye Hasira walipokwenda Barabarani kutoa wito wa kuondolewa kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa ambao walituhumiwa kutowalinda raia dhidi ya mashambulio mabaya ya waasi.

Kufuatia ghasia hizi, Jumatano Msemaji wa MONUSCO aliibuka kujibu hoja za maandamano akisema "Tuko hapa kwa mwaliko wa Serikali ya DRC Kongo, Sio sisi ambao tunaamua tubaki." Mathias Gillman

MONUSCO iliingia kulinda Amani DRC Kongo mapema mwanzoni 2010 na mpaka sasa ina wanajeshi zaidi ya 12,000 waliopelekwa nchini humo huku wengi wao wakiwa mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri wa Madini.

Mashariki mwa DRC Kongo ni eneo ambalo hali yake ni tete zaidi kwani iko chini ya zaidi ya vikundi 100 vya waasi ikiwa ni pamoja na Kikosi cha Allied Democratic Forces (ADF).

ADF ilianza miaka ya 1990 Magharibi mwa Uganda ikikusudia kuanzisha uongozi wenye misingi ya dini ya uislam.

Mnamo Machi 19, UN ilisema kuongezeka kwa Mashambulio ya ADF tangu kuanza kwa Mwaka kumeua zaidi ya watu 200 na kulazimisha 40,000 kukimbia Makazi yao.