Habari

Djibouti: Boti Yapinduka na Kuua Wahamiaji 34

Manusura wa mkasa huo waliripoti kwamba mashua hiyo kutoka Yemen ikiwa na idadi ya abiria 60 ilipinduka saa 4:00 asubuhi baada ya kukumbana na dhoruba kali baharini

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti vifo vya wahamiaji 34 waliofariki baada ya boti waliyokuwa wamepanda kupinduka na kuzama katika pwani ya Djibouti leo Jumatatu, Aprili 12, 2021.

Manusura wa mkasa huo waliripoti kwamba mashua hiyo kutoka Yemen ikiwa na idadi ya abiria 60 ilipinduka saa 4:00 asubuhi baada ya kukumbana na dhoruba kali baharini.

Mkurugenzi wa IOM wa Mashariki na Pembe ya Afrika, Mohammed Abdiker ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter juu ya mkasa huo, "Wahamiaji 34 wamefariki kutoka Pwani ya Djibouti baada ya boti yao kupinduka. Wahamiaji hao walikuwa wakisafirishwa kinyemela. Janga hilo la pili kutokea ndani ya miezi 2. mnamo Machi watu 20 walifariki na majeruhi kadhaa. ”

Boti hiyo ilipinduka baharini kaskazini mwa mji wa bandari wa Obock, eneo kuu la usafirishaji wa maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika katika eneo hilo aambao huwa wanataka kufika Ghuba.

Maafisa hao walisema kwamba manusura wapo hospitali wakipokea matibabu.

Wayemen wanakimbilia Afrika na maeneo mengine mbali na nyumba zao ili kukimbia vita. Inaaminika kwamba maelfu ya wahamiaji wamekwama nchini Yemen, ambapo mzozo wa miaka mingi umesababisha makumi ya maelfu ya maisha na mamilioni ya watu kuhama makazi yao.