
Shirika la afya duniani, WHO
hapo jana limeridhia mpango wa chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca
kuanza kusambazwa kwenye mataifa maskini ikiwa ni baada ya kuithibitisha na
kuona inafaa kwa dharura. Mataifa ya kipato cha chini na kati yanatarajiwa
kupata dozi ya kwanza ya chanjo hiyo mwishoni mwa mwezi Februari, ikiwa ni sehemu
ya mpango wa kimataifa wa mgawanyo wa chanjo, COVAX. Shirika hilo linataraji
kupeleka dozi milioni 336 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka na hadi
bilioni 2 ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba.
Covax ilizinduliwa mnamo
Aprili 2020 na inaongozwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), pamoja na Umoja
wa kushughulikia Chanjo Ulimwenguni. Covax inajulikana kama Covid-19 Vaccines
Global Access Facility.
Akionyesha ukosefu wa usawa
mnamo Januari, mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema zaidi ya dozi
milioni 39 zimetolewa katika nchi zisizopungua 49, wakati 25 tu zikielekezwa
katika moja ya nchi zenye kipato cha chini.
Ukosefu huo wa usawa
unatarajiwa kuendelea, kwani utafiti unaonyesha vipimo vingi vya chanjo
vimenunuliwa na nchi zenye kipato cha juu.
Nchi zenye kipato cha juu kwa
sasa zina chanjo zilizothibitishwa zipatazo bilioni 4.2, wakati mataifa ya
kipato cha chini yana dozi milioni 670 tu kulingana na utafiti wa Kituo cha
Ubunifu wa Afya cha Duke.
Mpango wa Covax ni nini?
Covax imepanga kuhakikisha nchi maskini na za kipato cha kati zinazopokea sehemu kubwa ya chanjo.Covax inatumai kuwa, ifikapo mwisho wa 2021, zaidi ya dozi bilioni mbili zitakuwa zimesambazwa nchini kote ulimwenguni huku dozi zipatazo bilioni1.8. zikitarajiwa kuelekezwa kwenye nchi maskini zinazohusika katika mpango huo, zikiwa karibu 20% ya watu wao.
Leave a comment