Habari

BURIANI MAGUFULI: Historia Fupi ya Maisha na Nyakati za Hayati Dokta John Pombe Magufuli

Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufariki akiwa madarakani.

 

Rais Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefariki Dunia Machi 17 majira ya saa 12 jioni katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena jijini Dar es Salaam kufuatia maradhi ya moyo.

 

Akitangaza kifo hicho Makamu wa Rais, Samia Suluhu ametangaza siku 14 za maombolezo.

 

Wizara ya Habari ya Serengeti Post inaungana na Watanzania pamoja na wote walioguswa na msiba popote duniani kuomboleza msiba huu mzito.

 

Serengeti Post imekuletea kwa ufupi historia kuhusu uongozi wa Rais Magufuli.

 

- Ni Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyetumikia nafasi yake kwa muda mfupi zaidi. Alihudumu kipindi chake cha kwanza cha miaka 5 na muhula wa pili alidumu kwa miezi 5.

- Ni Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufariki akiwa madarakani.

 

Hayati Rais Magufuli ni moja ya Watanzania watano waliopata nafasi ya kuwa viongozi wakuu wa nchi tangu Tanzania ilipopata uhuru Disemba 9, 1961. Mwaka 2015 Rais Magufuli alikuwa changuo la Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuteuliwa kuwania nafasi ya Urais. Rais Magufuli ambaye alipata upinzani mkali kutoka kwa Edward Lowasa wa CHADEMA aliingia kwenye kampeni kwa kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu akiwaaminisha wananchi kurejesha uwajibikaji wa viongozi na taasisi za serikali katika kuharakisha maendeleo.

 

Magufuli alishinda nafasi ya Urais kwa asilimia 58, ikiwa ni ushindi mwembamba zaidi katika historia kwa Rais kuingia madarakani, na aliapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Novemba 5, 2015. Rais Magufuli aliingia madarakani kwa mshindo akihimiza zaidi uwajibikaji wa watendaji na taasisi za serikali. Katika siku 100 za awali za Urais wake, nchi nyingi za Afrika na duniani kote na hata baadhi ya wapinzani wake walimsifu kwa namna ya uongozi wake.

 

Baadaye, Magufuli alikosolewa sana kwa aina yake ya uongozi ambapo Azaki za Kiraia, vyombo vya habari na vyama vya upinzani viliuita utawala kandamizi na usiozingatia haki na sheria.

 

Oktoba mwaka 2020 Magufuli alichaguliwa kwa muhula wa pili kwa asilimia 84 katika uchaguzi uliogubikwa na malalamiko ya wizi wa kura, uminywaji wa upinzani kwa kutumia vyombo vya dola na matumizi ya nguvu na kuzuiliwa kwa baadhi ya mikutano ya hadhara. Rais Magufuli ametumikia muhula wake wa pili kwa muda wa miezi mitano pekee kabla ya umauti kumfika.

 

Baadhi ya mambo makubwa yaliyompatia sifa Magufuli wakati wa uongozi wake ni pamoja na dhima yake ya kukuza uchumi wa Tanzania kupitia viwanda na alijikita katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli, madaraja, kufufua shirika la ndege la taifa, Air Tanzania  na ukali kwa watendaji aliowatathmini kuwa wazembe. Vilevile, ujenzi wa miradi ya umeme kama mradi maarufu wa bwawa la umeme la Nyerere (zamani Stiglers) na madaraja ya juu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli pia alipata sifa kwa kuchukua hatua za papo kwa papo dhidi ya watendaji wa serikali waliotuhumiwa kufanya makosa.

 

Magufuli alivuma pia kwa kuwa kiongozi mwenye msimamo, alisimamia maamuzi yake hata yale ambayo yalikuwa kinyume na ilani ya Chama cha Mapinduzi, sera, sheria na hata Katiba ya Nchi. Rais Magufuli alifanya maamuzi mengi ambayo hayakutarajiwa na wengi kama vile kupiga marufuku mikutano ya hadhara, kuingia katika mgogoro wa kimaslahi dhidi ya Barrick Corporation na hata ujenzi wa Bwawa la Umeme la Nyerere. Wengi wanamzungumzia kama kiongozi aliyekuwa na uthubutu mkubwa.

 

Kwa kiasi kikubwa, alifanikiwa kuwa sauti kuu ya nchi kama kiongozi namba moja. Alijaribu kwa namna nyingi kuzuia upinzani dhidi yake. Vyombo vya habari, Azaki za Kiraia, vyama vya upinzani na wakosoaji vilitulizwa kupitia sheria na aina nyingi za vitisho.

 

Aliitwa majina mengi kama tingatinga, jiwe, chuma na kadhalika.

 

Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 huko wilayani Chato mkoani Geita. Alianza maisha kama mwalimu wa kemia katika shule ya Sekondari Sengerema mwaka 1982 hadi 1983 na baadae alikua mkemia katika chama cha ushirika cha Nyanza. Aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 1995 baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Chato na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi. Mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Makazi, Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na mwaka 2010 hadi 2015 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

 

Kwa upande wa elimu, Magufuli alipata Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006-2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 1991 – 1994 alipata shahada ya uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza. Mwaka 1985 – 1988 alisoma shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisoma Kemia na Hisabati. Mwaka 1981 – 1982 alisoma diploma ya Chuo Kikuu cha Mkwawa akisoma masomo ya Kemia na Hisabati.