Habari

Brazil Yaripoti vifo 1,641 Vilivyotokea Ndani ya Siku moja Kutokana na Janga la Corona

Magavana wa majimbo nchini humo wameamua kuungana pamoja ili kununua chanjo baada ya serikali kuu kuonekana kutochukulia uzito suala la ununuzi wa Chanjo

Watu wapatao 1,641 walifariki kutokana na COVID-19 Jumanne ya Machi 2, kulingana na data ya Wizara ya Afya nchini humo huku idadi hiyo ikitajwa kuwa ni kubwa ikilinganishwa na vifo 1,595 vilivyotokea kwa siku moja mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka 2020.

Nchi hiyo ya America ya Kusini yenye idadi ya watu milioni 212 inakabiliwa na wimbi jipya la maambukizo ya virusi vya Corona huku hospitali zikionekana kulemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Zaidi ya watu 257,000 wamefariki kutokana na corona nchini Brazil na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi na janga la virusi vya Corona baada ya Marekani.

Magavana wa majimbo nchini humo wameamua kuungana pamoja ili kununua chanjo baada ya serikali kuu kuonekana kutochukulia uzito suala la ununuzi wa Chanjo.

Brazil imekua ikilegalega katika kutekeleza sera za kujikinga na janga hili huku majingo yakiwa hayana muitikio wa pamoja katika kupambana vita hivyo vikiongozwa na Rais Jair Bolsonaro ambaye amekuwa akipuuza na kudhihaki hatua zilizowekwa ili kujikinga na mashambulizi ya janga hilo.

Wiki iliyopita, Bolsonaro alidharau utumiaji wa barakoa, akisema vinaweza kusababisha maumivu ya kichwa huku akitishia pia kukata ufadhili kwa miji inayoteleza sera ya marufuku ya kutoka nje.