Habari

Mfahamu Marehemu Balozi Kijazi

Balozi Mhandisi John Kijazi amefariki akiwa ameacha mke wake, na watoto watatu

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano Ikulu, Balozi Mhandisi John William Herbert Kijazi amefariki Februari 17 majira ya saa tatu na dakika kumi usiku katika hosptali ya Benjamin Mkapa akiwa anapatiwa matibabu.

Taarifa huyo inaeleza kuwa taratibu za mazishi ya Kiongozi huyo zitatangazwa hapo baadae. 

Lakini Balozi John William Kijazi ni Nani?

Amekuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 - 2016 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.

Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.

Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo.

Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.

Balozi Mhandisi John Kijazi amefariki akiwa ameacha mke, Fransisca Kijazi pamoja na watoto watatu, David, Emmanuel na Richard Kijazi.