Habari

Afrika Kusini: Mfalme wa Wazulu, Goodwill Zwelithini Aaga Dunia

Mfalme Zwelithini alijivunia ushawishi mkubwa kati ya mamilioni ya Wazulu kupitia sherehe zake za kimila na kiroho licha ya uongozi wake kuisha tija ndani ya Afrika Kusini ya kisasa

Goodwill Zwelithini, Mfalme aliyeheshimiwa na Wazulu wa Afrika Kusini, amefariki akiwa na umri wa miaka 72 baada ya kukaa wiki hospitalini akiwa anatibiwa ugonjwa wa kisukari.

Mfalme Zwelithini alijivunia ushawishi mkubwa kati ya mamilioni ya Wazulu kupitia sherehe zake za kimila na kiroho  licha ya uongozi wake kuisha tija ndani ya Afrika Kusini ya kisasa.

"Ni kwa masikitiko makubwa ninaujulisha umma juu ya kufariki kwa Mfalme wake Goodwill Zwelithini… Mfalme wa taifa la Zulu," ikulu ilisema taarifa iliyosainiwa na Mangosuthu Buthelezi, mwanasiasa mkongwe mwenye nguvu ambaye pia ni mkuu wa Kizulu.

Mfalme alilazwa hospitalini mwezi uliopita kwa ugonjwa wa kisukari.

"Cha kusikitisha, wakati bado akiwa hospitalini, afya yake ilizidi kuwa mbaya na baadaye alifariki mapema asubuhi."

"Kwa niaba ya Familia ya Kifalme, tunashukuru taifa kwa maombi na msaada katika kipindi hiki kigumu zaidi." ilieleza taarifa hiyo

Zwelithini ni mzaliwa wa Nongoma, mji mdogo kusini mashariki mwa mkoa wa Kwa-Zulu Natal, Zwelithini alipokea kijiti cha ufalme akiwa na umri wa miaka 23 kipindi cha vita ya ubaguzi wa rangi mnamo mwaka 1971 ikiwa ni miaka 3 baada ya kifo cha baba yake.